Uchambuzi wa riwaya ya Barua Ndefu Kama Hii
KITIVO CHA ELIMU
IDARA YA KISWAHILI
JINA LA KOZI : RIWAYA YA KISWAHILI NA TAHAKIKI
MSIMBO WA KOZI : EDK 07402
INAWASILISHWA KWA : Madam. S. LEBABU
INAWASILISHWA NA : SOMEKE B. KIBANDIKO
NAMBA YA USAJILI : 2018100202
Swali
Kwa kutumia riwaya moja uliyosoma, Chambua mambo yafuatayo
Uchambuzi wa fani na maudhui katika Riwaya teule
Nadharia za Uchambuzi wa Riwaya
Riwaya ya Kiswahili namapokeo ya kiasili
Athari za Utamaduni wa nje katika Riwaya ya Kiswahili
TAREHE YA KUWASILISHA 03-JULY-2020
UTANGULIZI
Dhana ya Riwaya imeweza kuelezwa na wataalamu mbalimbali. Mulokozi (1996) anaeleza kuwa, Riwaya ni masimulizi marefu ya kinathari yaliyochangamana kiasi, yenye kuzungumzia tajriba ya maisha ya binadamu kwa ubunifu.
Kwa mujibu wa Wamitila (2002) na Senkoro (2011), wanasema, riwaya ni kisa mchangamano ambacho huweza kuchambuliwa na kupimwa kwa mapana na marefu kifani na kimaudhui.
Madumulla (2009) anasema, riwaya ni masimulizi ya kubuni yaliyo katika mtindo wa kubuni yakisawiri mtindo maalumu na maudhui maalumu.
Kwa ujumla naweza kusema, riwaya ni utanzu mojawapo wa fasihi andishi wenye mtindo wa kinathari ulionyumbuka kifani na kimaudhui.
Kwa kutumia riwaya ya Barua Ndefu Kama Hii. Iliyoandikwa na Mariama Ba, nitachambua au kuhakiki Athari za utamaduni wa nje katia riwaya ya Kiswahili, Riwaya ya Kiswahili na mapokeo ya kiasili, Nadharia za uchambuzi wa riwaya, na uchambuzi wa fani na maudhui katika riwaya hii.
A: UCHAMBUZI WA FANI NA MAUDHUI
Kabla ya kuanza kuchambua vipera vya fani na maudhui ni vyema kueleza dhana ya fani na maudhui. Kwa kuanza na uchambuzi wa fani katika riwaya ya “Barua Ndefu Kama Hii” ni kama ifuatavyo:-
FANI
Fani ni mbinu mbalimbali azitumiazo mwandishi (mtunzi) wa kazi ya fahisi ili kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa jamii.
Fani ndiyo bahasha inayobeba maudhui iliyokusudiwa na mwandishi. Mbinu hizo hujibainisha katika vipengele mbalimbali kama vile; Muundo, Mtindo, utumizi wa Lugha, Mandhari na wahusika. Mwandishi wa riwaya hii ameweza kuvitumia vipengele hivi kama ifuatavyo:-
Muundo; muundo ni mpangilio wa visa na matukio katika kazi ya fasihi . Mwandishi wa riwaya hii, Mariama Ba ametumia Muundo changamano (Rukia) kwani ameanza kwa kuelezea kifo cha Modu, hadi mazishi yake, kisha anaanza kutueleza visa vilivyojiri wakati wa uhai wa Modu huku akirejerea matukio mbalimbali yaliyopita likiwemo lile la chanzo cha kutelekeza familia yake na hatimaye yaliyoendelea baada ya msiba kuisha katika familia ya Modu na Ramatulayi. Hivyo riwaya hii ya “Barua Ndefu kama Hii” imetumia muundo wa Rukia (Changamano).
Mtindo; mtindo ni mbinu aitumiayo mtunzi (mwandishi) wa kazi ya fasihi ili kujitofautisha na waandishi wengine. Mbinu hiyo inaweza kuwa, masimulizi (monolojia), majibizano (Dayolojia), matumizi ya nafsi mbalimbali, matumizi ya tanzu nyingine za fasihi katika utanzu mmoja, matumizi ya maandishi mbalimbali kama vile insha, magazeti, matangazo au barua, na kadhalika.
Katika riwaya ya “Barua Ndefu kama Hii” mwandishi ametumia mtindo wa masimulizi (Monolojia) ambapo amemtumia mhusika, Ramatulayi kusimulia visa na matukio mbalimbali yanayomkumba yeye kama mwanamke, familia yake pamoja na jamii yake kwa njia ya barua. Pia mwandishi ametumia mtindo wa Barua ya Kirafiki ambapo riwaya nzima ni barua ya Ramatulayi aliyomwandikia rafiki yake, Aisatu. Ndani ya barua hii kuna barua tena ambayo Ramatulayi alimwandikia Dauda Diengi (Sura ya 21. Uk 92).
Vilevile mwandishi ametumia mtindo wa matumizi ya nafsi zote tatu wakati nafsi ya tatu umoja ikiwa imetawala katika riwaya hii. Kwa kiasi kidogo sana, mwandishi ametumia mtindo wa majibizano. Mtindo huu unajidhihirisha katika sura ya 25 (Uk 115) ambapo Farmata anamhoji Ibrahima kama ifuatavyo,
“Ni kweli wewe ndiwe wa kwanza?
Ndiyo!
Badi ….” (Uk 115).
Pia mazungumzo ya Imamu na Tamsiri (Uk. 48). Vilevile mwandishi ametumia mtindo wa sura fupifupi ambazo jumla ziko sura 27. Hivyo, Mwandishi ametumia mitindo mbalimbali kama ilivyoelezwa hapo juu.
Mandhari; mandhari ni sehemu ambapo matukio na visa mbalimbali hutendekea katika kazi ya fasihi. Mandhari ya kazi ya fasihi inaweza kuwa halisi au ya kubuni (sio halisi) Katika riwaya ya “Barua Ndefu kama Hii” mwandishi Mariama Ba ametumia Mandhari halisi ya kiafrika hasahasa ya Kisenegali ambapo ameonesha baadhi ya maeneo na miji inayopatikana katika nchi ya Senegali (Senegal). Mfano, ameonesha maeneo kama vile; Santa – luui amabayo ni makao makuu Mapya ya Senegali, Uakamu, Thiaroye, Dakar, Faleni Yoffu (uwanja wa ndege wa Senegali), Ngori na Pwani ya Almadi( Sura ya 9). Hivyo, mandhari katika riwaya hii ni mandhari halisi ambayo inafikika na kuonekana kiuhalisia.
Wahusika, wahusika ni jumla ya viumbe hai au visivyo hai ambavyo hutumiwa na waaandishi (mtunzi) kutenda kuendenda au kuiga matendo, mienendo na tabia halisi za binadamu halisi katika kazi ya fasihi ili kufikisha ujumbe uliokusudiwa na mwandishi (mtunzi) katika jamii.
Katika riwaya ya “Barua Ndefu Kama Hii” mwandishi Mariama Ba ametumia wahusika mbalimbali waliobeba ujumbe mzito aliokusudia uifikie jamii yake. Wahusika hao ni kama ifuatavyo:-
1. Ramatulayi. Huyu ni mhusika mkuu ambaye ametumika kuibeba dhamira kuu katika riwaya hii. Mhusika huyu ni mwanamke msomi ambaye ni mwalimu, ni mke wa Modu Falli ambaye alitelekezwa na mume wake (Modu) miaka mitano kabla ya kifo cha mumewe (Modu) baada ya mume wake kuoa mke wa pili (Binetuu). Ni mvumilivu mwenye mapenzi ya dhati, pia mwanamke anayetetea haki za wanawake katika jamii yake. Ni mama mlezi wa familia yake yenye watoto 12. Anajifunza kutokana na makosa yake. Anafaa kuigwa na jamii.
2. Modu Falli
Huyu ni mume wa Ramatulayi, alimtelekeza mke wake baada ya kuingiwa na tama ya mitahala na kumuoa Binetuu. Alifariki kwa ajali ya gari. Alikuwa ni msomi aliyetetea haki za wafanyakazi na kuwashauri wasigome wakati wa uhai wake. Alitumia vibaya mali ili kuwaridhisha mke mdogo Binetuu na wakwe zake, Bibi mama – Mkwe. Alikuwa rafiki wa karibu wa Maudo Ba. Anafaa kuigwa kwa machache lakini hafai kuigwa kwa tabia za utelekezaji wa mwanamke na kutumia vibaya mali.
3. Maudo Ba.
Huyu ni mwanamme rafiki wa Karibu na modu falli. Ni daktari makini mwenye kuipenda kazi yake. Alikuwa mume wa Aisatu kabla ya kuachwa na Aisatu kwa sababu ya kumuoa Zainabu mdogo (Nabu mdogo) kwa shinikizo la mama yake Shangazi Nabu. Anafaa kuigwa kwa umakini wa kazi yake, lakini hafai kuigwa kwa kukosa maamuzi binafsi.
4. Aisatu
Huyu ni mwanamke ambaye ni shoga wa karibu wa Ramatulayi, anamapenzi ya dhati kwa rafiki yake na familia ya Ramatulayi. Alikuwa mke wa Maudo Ba. Ni mwanamke msomi ambaye ni mkalimani. Anafanya kazi katika ubalozi wa senegali huko Marekani. Ametokea katika familia ya mfua vyuma. Alimuacha Maudo Ba baada ya kuoa mke wa pili. Ni mpiganiaji wa haki za wanawake. Anafaa kuigwa na jamii.
5. Dauda Diengi
Huyu ni mwanamme msomi na mbunge (mwanasiasa) alitumia siasa yake kutetea haki za wanawake na maendeleo ya nchi yake. Anamapenzi ya dhati kwani alimpenda sana Ramatulayi ingawa hakukubaliwa naye. Alihitaji kumuposa Ramatulayi baada ya kifo cha Modu. Lakini Ramatulayi hakuwa tayari kwa sababu ya maumivu ya kutelekezwa na Modu. Ni mwenye juhudi na si mwepesi wa kukata tama. Ana busara anafaa kuigwa na jamii.
6. Binetuu
Hutu ni mke mdogo wa Marehemu Modu Falli. Aliachishwa masomo na mzazi wake Bibi Mama – mkwe ili aolewe na Modu wakati alipokuwa anasoma kidato cha sita pamoja na Daba binti wa Modu. Ndiye chanzo cha Modu kumtelekeza mke wake, Ramatulayi. Alikuwa ni mtoto wa masikini aliyetumia uzuri wa sura yake kumnasa Modu. Anapenda starehe na anasa. Hafai kuigwa na jamii.
7. Daba
Huyu ni binti mkubwa wa Modu Falli na Ramatulayi. Ni msomi ambaye pia ni mtetezi wa haki za wanawake. Ana busara na anajitambua. Alikuwa rafiki wa Binetuu kabla Binetuu hajaolewa na Modu(baba yake). Ni mshauri mzuri. Anamapenzi ya dhati na aliolewa na Abuu. Anafaa kuigwa na jamii.
8. Wahusika wengine
Shangazi Zainabu (Nabu) mama wa Maudo Ba.
Aisatu Somo (Binti wa Ramatulayi na Modu)
Zainabu (Nabu) Mdogo – Binti wa kaka yake shangazi Nabu
Farmata-Malenga mtabiri mshirikina.
Tamsiri – kaka wa Modu
Farba Diufu – Kaka wa shangazi Nabu
Bibi Mama - mkwe – Mama wa Binetuu
Abuu – Mume wa Daba
Ibrahima Salli – Kijana aliyempa mimba Aisatu mdogona kuahidi kumuoa
Maudo Falli – Kijana wa Ramatulayi na Modu, n.k
Utumizi ya lugha, utumizi ya lugha ni namna ambavyo mwandishi anavyotumia lugha kisanaa ili kufikisha ujumbe wake kwa jamii husika. Katika riwaya ya “Barua Ndefu kama Hii” mwandishi Mariama Ba ametumia lugha fasaha na ya kawaida inayoeleweka, iliyojaa misemo, nahau, methali, tamathali za semi, mbinu nyingine za kisanaa na Taswira mbalimbali kama ifuatavyo:-
Nahau /misemo
Katika riwaya hii mwandishi ametumia nahau na misemo mbalimbali kwa mfano
“Makofi yanayofaulu kuwaweka sawa watoto wadogo huwa yanawaudhi vijana wakubwa” (uk. 102).
“Maji na mchanga vimechanganyikana na kutengeneza tope” (uk. 110)
“Kwenda ulikoelekea upepo” (uk. 103)
Methali
Mwandishi wa riwaya hii ametumia methali kama vile:-
“Mama mwenye mtoto hana muda wa kutalii bali wa kufa nao” (sura ya 23, uk 101)
“Tumbo unapolipa chakula hujaa bila wewe kujua” (sura 23.) uk 104)
“kukosana kunaweza kukuletea bahati kwa baadaye” (uk. 54).
Tamathali za semi
Katika riwaya hii mwandishi Mariama Ba ametumia tamathali za semi kama ifuatavyo
Tashibiha
Katia riwaya hii tamathali ya ulinganishaji wa vitu kwa kutumia viunganishi imetumika kwa mfano
“Suruali hufanya maungo yaliyonenepa ya mwanamke wa Kafria yajitokeze hasa matako yaliyoviringika kama tufe” (sura ya 23. Uk 103)
“Hasira yangu ikawaangukia kama radi” (uk 103)
“…. Na msichana mwenye umri sawasawa na mimi” (uk 52)
“Kisha nikauliza kwa kilio kikali kama cha mnyama mkali…” (uk 48)
“Utadhani maneno yalimkaa kama makaa ya moto kinywani” (uk 48).
Mubalagha /chuku
Pia mwandishi ametumia mubalagha katika riwaya hii
Mfano
“Mtunda yalikuwa yanachumika hali umeketi chini (sura ya 9)
“Kisha nikauliza kwa kilio kikali kama cha mnyama mkali aliyezingirwa na wawindaji” (uk 48) n.k.
Tashihisi
Tashihisi pia imeonekana katika riwaya hii, mfano:-
“Ng’ombe walikatisha njia taratibu huku wamenunanuna” (uk 36)
“Damu iliyoganda kutoka kwenye majeraha, ilichora mabaka meusi kwenye udongo” (Uk. 106).
Lakabu
Mwandishi wa riwaya hii ametumia lakabu mbalimbali. Mfano
“Simba jike” (Uk 94) jina alilopewa la Matulahi huko mjini baada ya kuwakataa wanaume na kujitegemea.
“ tumbotumbo” (uk. 52) jina alilopewa Modu na Binetuu. n.k
Tafsida
Matumizi ya tafsida yameonekana katika baadhi ya sehemu za riwaya hii.
“Mabalaa” (Matatizo) Uk. 108.
Wakati umepita sana (Amezeeka), Uk.48
“Nakuonea gele” (Nakuonea wivu) Uk. 118.
Stiari
Sitiari zilizotumika katika riwaya hii ni kama vile
“Barabara ni chambo kikubwa sana” (uk 106)
“…… utadhani ni mashetani” (uk. 106)
Mbinu nyingine za kisanaa.
Katika riwaya hii, mwandishi pia ametumia mbinu mbalimbali za kisanaa kama vile
Takriri
Mfano
“Nyamaza nyamaza! Acha ! Acha!” (Uk 78)
“Naam; Naam” (Uk 48)
“Acha, Ramatulayi, Acha” (Uk 87)
Tashtiti
Katika sehemu nyingi za riwaya hii, mwandishi ametumia mbinu ya tashititi kwa mfano.
“Leo hamna wageni?” (Uk. 86)
“Je niyakubalie moja kwa moja mapendekezo yake?” (uk. 115)
“Aliwezaje peke yake kukaa na siri yake?” (uk 113)
“Ni mume mwema?” (Uk 90)
“Je tayari umeshakutana na mkewe wa pili?” (Uk. 52).
Mdokezo
Mfano
“Angalia … utajuta kuvunjika sehemu Fulani kama yaliyompata kaka yako” (uk. 107)
“Labda wale watatu walishajua tayari… wakakaa kimya kwa muda mrefu… kisha hao! Wakatoka ….” (Uk. 119)
Nidaa
Mfano
“….. Badala ya kung’aa pepepe!” (Uk. 103)
“Lo!... (uk . 101)
“Ama kweli, watoto !./…..” (uk. 106)
“Ha!” (uk. 108)
“kupendana!” (uk. 120).
Majalizo
Mfano
“Unataka meza, sahani, kiti, uma….” (uk. 121)
Tanakari sauti
“akashikwa na kwikwi” (uk 113)
Taswira
Katika riwaya hii kuna matumizi ya taswira mbalimbali kama vile
Taswira zinazoonekana
Mfano
Chale mbili zilizotengana – usaliti (sura ya 13)
Jani lililopeperushwa – kuterekezwa (sura 16)
Simbi – huonesha tukio mtu au vitu vitakavyotokea (kutabiri) (Uk. 109).
Taswira za hisi
Mfano
“Damu iliyoganda kutoka kwenye majeraha, ilichora mabaka meusi kwenye udongo yasiyopendeza kutazamwa wala kunuswa” (uk 106)
Taswira za kufikirika
Mfano
“Uchungu ukanijaa rohoni … nikajisikia mwili mzima umechemka… nikama na mung’unyamung’unya ulimi wangu” (uk 110).
MAUDHUI
Maudhui ni jumla ya mawazo yote yanayozungumzwa pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo. Katika riwaya ya “Barua Ndefu kama Hii” nitavichambua vipengele vya maudhui ambavyo ni Dhamira, Migogoro, Ujumbe, falsafa na mtazamo /msimamo kama ifuatavyo:-
Dhamira
Dhamira ni wazo kuu au mawazo makuu yanayojitokeza katika kazi ya fasihi ambayo mwandishi amekusudia kuyafikisha kwa jamii. Katika riwaya hii, mwandishi ameweza kuiweka dhamira kuu ni Ukombozi wa Mwanamke katika Nyanja zote za kiuchumi, kisiasa, kijamii , kifikra na kiutamaduni.
Ukombozi wa mwanamke kijamii, mwandishi wa riwaya hii ameweza kuibua dhamira ya ukombozi wa wanawake kwa kuonesha kuwa, wanawake, wanatakiwa kuwa na haki sawa na wanaume katika jamii. Haki hizo ni kama vile, elimu, shughuli za nyumbani, malezi ya familia na heshima katika jamii sawa na wanaume. Mariama Ba ametumia baadhi ya wahusika kuonesha namna ambavyo mwanamke anatakiwa kupewa haki hizo na pia ametumia baadhi ya wahusika kuionya jamii iondokane na mtazamo hasi wa kuwaona wanawake kama kiumbe dhaifu. Mfano mzuri wa kuonesha haki sawa katika jamii hasa katika shughuli za kifamilia, mwandishi amemtumia Abu mume wa Daba ambaye alikuwa anamsaidia Daba (mke wake) shughuli za ndani kama vile kupika; mwandishi anasema;
“Daba hazidiwi na kazi nyumbani mumewe anajua kupika wali kama yeye mwenyewe…. Husema:- Daba ni mke wangi si mtunmwa wangu wala mjakazi wangu” (uk. 99).
Hii inaonehsa usawa wa majukumu ya kifamilia kati ya mwanamume na mwanamke katika jamii.
Pia mwandishi amewatumia wahusia wanawake kama vile; Ramatulayi, Aisatu, Nabu Mdogo, na Daba kama wanawake wasomi wanaojitambua ili kuonesha haki ya wanawake kupata elimu na hivyo kuwakomboa wanawake kielimu katika jamii. Hivyo dhamira hii ya ukombozi wa mwanamke kijamii imejadiliwa kwa urefu na mapana sana katika riwaya hii.
Ukombozi wa mwanamke kisiasa.
Mwandishi Mariama Ba, ameweza pia kujadili dhamira ya ukombozi wa mwanamke kisisa kwa kudai haki ya usawa katika shughuli za siasa kama vile Bunge na utawala. Mwandishi amemtumia mhusika Dauda Diengi kama mwanamme anayeungana na wanawake kutetea haki ya usawa bungeni kama anavyomwambia Ramatulayi.
“Ujamaa ambao ni kiini cha madai yako, ndilo lengo la matumaini yangu ya dhati….” (uk. 86).
Vilevile Ramatulayi anadai haki ya wanawake katika ngazi ya utawala. Anasema
“Lini tutapata mwanamke wa kwanza awe waziri ….?” (Uk 82).
Hivyo, mwandishi amedhamiria kumkomboa mwanamke kisiasa kipitia wahusika Dauda Diengi na Ramatulayi waliobeba dhamira ya ukombozi wa mwanamke kisiasa.
Ukombozi wa Mwanamke kiuchumi
Dhamira ya ukombozi wa mwanamke kiuchumi imejitokeza katika riwaya hii ambapo mwandishi amewatumia wahusika Ramatulayi na Aisatu kama wanawake ambao wameajiriwa na wanauwezo wa kujimudu kiuchumi na hata kuyaendesha maisha yao. Mwandishi anaonesha kuwa ajira ni mbinu moja wapo ambayo inaweza kumkomboa mwanamke kiuchumi. Hivyo anawahimiza wanawake wasome kwa bidii ili waweze kupata ajira na waweze kujikomboa kiuchumi.
Vilevile, mwandishi ameonesha mbinu nyingine ya mwanamke kujikomboa kiuchumi ni kujiari mwenyewe badala ya kusubiria kuajiriwa. Mfano mzuri katika Riwaya hii, mwandishi amemtumia Aisatu ambaye alikuwa amejiari katika kazi za mikono za usonara ambazo zilikuwa zinamuingizia kipato kabla ya kuajiriwa katika ubalozi wa senegali huko marekani. Hivyo, mwandishi ameonesha dhamira ya ukombozi wa mwanamke kiuchumi.
Ukombozi wa mwanamke kiutamaduni
Mwandishi wa riwaya hii pia ameonesha dhamira ya ukombozi wa mwanamke kiutamaduni kwa kumtumia mhusika Ramatulayi na Aisatu ambao ni mwanawake wailolelewa katika misingi ya imani ya kiislamu ambayo inaruhusu ndoa za mitahala. Aisatu anaamua kumuacha mume wake, Maudo Ba. Baada ya kuoa mwanamke wa pili (Nabu mdogo). Hii inaonesha kuwa Aisatu hakupendezwa na desturi hiyo ya mitaala.
Pia Ramatuliyi baada ya kufiwa na mume wake (Modu), Tamsiri mdogo wake marehemu Modu alitaka kumrithi Ramatulayi, Ramatulayi alipinga vikali suala hilo na kusema;
“Tamsiri, zitapike hizo ndoto zako za kutaka kuniposa” (uk. 78).
Hivyo mambo haya yanadhihilisha kuwa mwandishi alidhamilia kumkomboa mwanamke kuondokana na utamaduni ambao unamfanya atumike kama chombo cha kumstarehesha mwanamme.
Ukombozi wa Mwanamke Kifikira
Mwandishi pia ameweza kuonesha dhamira ya ukombozi wa mwanamke kifikra ambapo ametumia baadhi ya wahusika wenye fikra finyu ya maisha. Kwa mfano Binetuu, na Bibi mama – mkwe ambao wailishi kwa kutegemea bahati ya uzuri wa uso na maumbile ya mwili wa Binetuu.
Fikra kama hizo zinapingwa vikali na baadhi ya wahusika ambao mwandishi amewatumia kumkomboa mwanamke. Wahusika hao ni kama vile, Ramatulayi na Daba. Mwandishi anapiga vita tabia au fikra hasi kama walizokuwa nazo Binetuu na mama yake, Bibi mama – mkwe.
Anasema
“inawezekanaje mwanamke amharibie mwanamke mwenzake bahati yake” (uk. 95).
Vilevile, mwandishi anamalizia kwa kusisitiza kupitia mhusika Ramatulayi kuwa wanawake wanatakiwa waachane na fikra mbaya za kutumia miili yao kwa ajili ya kujipatia maisha mazuri kama anavyosema Ramatulayi.
“Nasisitiza kwamba mabinti zangu sharti watambue thamani ya miili yao” (uk. 118).
Hii ni kutokana na fikra ambazo zilijengeka miongoni mwa wanawake hasa mabiti wa mjini, kutumia uzuri na maumbile ya miili yao ili kuwanasa wanaume wenye pesa na maendeleo jambo ambalo lilipelekea kutelekezwa kwa ndoa nyingi ikiwemo ya Ramatulayi.
Dhamira nyingine
Nafasi ya mwanamke katika jamii, katika riwaya hii, mwanamke amechorwa kama ifuatavyo:-
Mwanamke kama mtu msomi na anayejitambua, mwandishi wa riwaya hii amechorwa mwanamke kama msomi na mtu anayejitambua anayepigania haki zae na uhuru wa maamuzi. Mfano mzuri wa wanawake wasomi walioonekana katika riwaya hii ni kama vile Ramatulayi ambaye ni mwalimu, Aisatu ambaye ni Mkalimani Nabu mdogo ambaye ni mkunga, na Daba mdogo ambaye amehitimu chuo kikuu miongoni mwa wengine.
Mwanamke kama mlezi wa familia. Pia katika riwaya hii, mwandishi amemchora mwanamke kama mlezi wa familia anayejali, kulinda, kutunza na kuipenda familia. Mfano mzuri ni Ramatulayi ambaye aliilea familia yake yenye watoto kumi na mbili bila kujali changamoto alizokutana nazo baada ya kutelekezwa na Modu Falli. Pia Aisatu ambaye aliamua kuondoka na watoto wake baada ya mume wake (Maudo Ba.) kuoa mwanamke wa pili.
Mwanamke kama mtu mwenye upendo wa dhati, mvumilivu, mwenye bidii, mchapakazi na mwenye busara. Katika riwaya hii mhusika mkuu Ramatulayi ameonekana kubeba sifa zote hizi kwa kuwa aliwapenda sana watoto wake. Pia alimpenda kwa dhati mume wake (Modu). Aliweza kuvumilia matatizo na changamoto za kimaisha zilizomkabili, alikuwa na busara na ndiyo mana alikuwa akipigania haki za wanawake katika jamii yake.
Vilevile, Ramatulayi, Nabu Mdogo, Aisatu, Daba na Aisatu mdogo walikuwa ni wanawake wachapakazi kwa kuwa walifanya kazi kwa bidii kulingana na kazi waliyokuwa wanaifanya.
Malezi na ndoa, mwandishi wa riwaya hii amejadili pia suala la malezi na ndoa. Kwa kuanza na malezi, mwandishi anaonesha kuwa suala la malezi ya familia ni jukumu la wazazi wote yaani mke na mume wala sio jukumu la mtu mmoja tu. Ameonesha namna jukumu hili linavyokuwa zito hasa pale mmoja wa walezi hao anapoamua kutelekeza jukumu hilo kwa mtu mmoja. Mwandishi amelionesha hili kupitia Ramatulayi ambaye aliachiwa jukumu la kuilea familia baada ya mume wake kumtelekeza jambo ambalo lilipelekea madhara makubwa kama vile, watoto wa kike (Diyinaba, Aramu na Yasini) kujiingiza katika kitendo cha kuvuta sigara (uk. 103), watoto kucheza hovyohovyo na kusababisha ajali ya kuvunjika mkono (uk. 107-110), na mtoto kupata mimba za utotoni (Aisatu mdogo (uk 110).
Pia kwa upande wa ndoa, mwandishi ameangazia matatizo mbalimbali yanayojitokeza katika suala la ndoa za mitaala ambazo zimepewa kibali katika imani ya dini ya kiisilamu. Mwandishi kupitia mhusika Ramatulayi, anaonesha kuwa hakuna haja ya kuoa ndoa za mitala ikiwa mke na mme wanaupendo wa kweli na wanatimiziana mahitaji yao katika ndoa. Pia anaonesha kuwa ndoa za mitala ni chanzo cha utelekezaji wa familia hasa mke wa kwanza. Mfano kwa Ramatulayi na Modu (Sura ya 13 na 14(.
Suala la mapenzi
Mwandishi wa riwaya hii ameweza kulijadili swala la mapenzi katika pande mbili, mapenzi ya kweli na mapenzi ya uongo (mapenzi ya dhati na yasiyo ya dhati). Kwa kuanza na mapenzi ya dhati mwandishi amelionesha swala hili kama ifuatavyo:-
Mapenzi ya dhati ya Ramatulayi na Aisatu. Mapezi haya yanajidhihirisha wazi toka mwanzo had mwisho wa riwaya hii, ambapo hawa wawili ni marafiki (shoga) ambao wanapendana sana hadi inafikia sehemu Aisatu anamnunulia Ramatulayi gari ili limsaidie kupeleka watoto shule. Ramatulayi na Aisatu wailpendana sana hata wakati wa shida walisaidiana kutatua changamoto. Urafiki wao ulianza tangu wakiwa wadogo unasoma hadi wilpokuwa watu wazima.
Mapenzi ya dhati ya Ramatulayi kwa Modu. Ramatulayi alimpenda kwa dhati Modu ambaye baadaye alimtelekeza jambo ambalo lilimfanya Ramatualayi aumie sana katika maisha yake yote.
Mapenzi ya dhati ya Ramatulayi na familia yake (Watoto wake) Ramatulayi anawapenda kwa dhati watoto wake na hivyo alikuwa tayari kupambana na hali yoyote ya kimaisha kuhakikisha watoto wake wako salama (uk. 101).
Mapenzi ya dhati ya Dauda Diengi kwa nchi yake, Dauda aliipenda nchi yake kwa dhati na alikuwa yupo tayari kupokea mawazo mazuri ya kimaendeleo ambayo yangeifanya nchi yake (Senegali) iendelee zaidi. (uk. 86).
Kwa upande wa mapenzi ya uongo, haya yamejibainisha wazi kama ifuatavyo:-
Mapenzi ya uongo ya Binetuu kwa Modu Falli Buinetu hakumpencda kwa dhati Modufali bali alijifaanya kumpenda ili atomize ndoto yake y kuwa namaisha maisha mazuri. Hivyo alipenda pesa alizokuwa nazo Modu(Uk.46).
Mapenzi ya uongo ya Modu Falli kwa Ramatulayi, Modu alijifanya kumpenda Ramatulayi kwa muda wa miaka 25 ya ndoa na baadaye akamtelekeza baada ya kumpenda Binetuu. (Uk. 47).
Suala la Demokrasia
Mwandishi wa Riwaya hii amegusia swala la demokrasia akihimiza demokrasia ya kweli. Dhamira hii ameiibua kupitia mazungumzo ya Ramatulayi na Dauda Diengi ambapo anataja kuwa ujamaa (usawa) ndio chanzo kikuu cha demokrasi ya kweli. Hii imejidhuhirisha katika ukurasa wa 86 na 87. Demokrasia ya kweli itakuwepo tu pale ambapo wanawake na wanaume watakuwa na nafasi sawa katika utawala na Bunge. Hivyo hii ni dhamira nyingine iliyoibuliwa katika Riwaya hii.
Dhamira ndogondogo
Mwandishi, Mariama Ba. Ameweza kuonesha dhamira ndogondogo amabazo ndizo zinazojenga dhamira kuu ya ukombozi wa mwanamke. Dhamira hizo ni pamoja na:-
Ajari na Kifo (Sura ya 1 na 24), Ubaguzi wa rangi (uk. 97), ubaguzi wa kijinsia (Uk. 85), mmomonyoko wa maadili (Sura ya 14), uvumilivu, Ugonjwa wa misongo ya mawazo kutokana na mapenzi (kutelekezwa) (Sura ya 14) n.k.
Migogoro
Migogoro ni mivutano au misuguano mbalimbali katika kazi ya fasihi, au kwa maana nyingine, migogoro ni hali ya kutokuelewana au kuhitilafiana baina ya pande mbili. Mfano, mtu na nafsi yake, mtu na mtu, mtu na kikundi cha watu au kikundi cha watu na kikundi kingine.
Katika riwaya hii ya “Barua Ndefu kama Hii” migogoro imeweza kujitokeza kama ifuatavyo:-
Mgogoro kati ya Ramatulayi na Modu Falli. Mgogoro huu umejitokeza katika sura ya 13 baada ya Modu Falli kupata mke wa pili na kuitelekeza familia yake. Ramatulayi pamoja na familia yake hasahasa binti yake, Daba, wanalaani vikali kitendo alichokifanya Modu.
Mgogoro kati ya Daba na Binetuu Mgogoro huu pia unajitokeza katika ukurasa wa 95, ambapo Daba alikwenda kurudisha mali za marehemu Baba yake baada ya kuchukuliwa na Binetuu na mama yake (Bibi mama – mkwe).
Mgogoro kati ya mwendesha pikipiki na vijana wa mtaani, mgogoro huu umeonekana baada ya kijana mwendesha pikipiki kuwagonga Aliuni na Maliki watoto wa Ramatulayi wakati wanacheza mpira kandokando ya barabara. Mgogoro huu ulitatuliwa baada ya Ramatulayi kumruhusu Yule kijana aondoke aende zake wakati vijana wa mtaani walipotaka wampige (uk. 105-106).
Mgogoro kati ya Aisatu na Maudo Ba. Mgogoro huu umejitokeza baada ya Maudo Ba kuoa mke wa pili (Nabu Mdogo) katika sura ya 12. Mgogoro huu hitimisho lake ilikuwa ni uamzi wa Aisatu kumuacha Maudo Ba, na mke wake mpya na kuondoka zake.
Mgogoro kati ya Aisatu mdogo na mama yake (Ramatulayi) mgogoro huu umejitokeza baada ya Aisatu mdogo (Somo) kupata Mimba wakati akiendelea na masomo. Mgogoro huu ulimalizika kwa kusamehe ambapo Ramatulayi aliamua kumsamehe binti yake kwa kumuita kijana muhusika (Ibrahima) kijana huyu alikiri na kukubali kumuoa Aisatu mdogo (somo) (uk. 110-115).
Mgogoro kati ya Maudo Falli (Kijana wa Ramatulayi) na mwalimu wake mgogoro huu umejitokeza baada ya mwalimu wa somo la Falsafa kuwa na upendeleo hasa ule wa rangi. Alimpendelea kijana wa kizungu (John – Klaudi) katika somo lake la Falsafa badala ya kumpatia Maudo Falli haki yakuwa wa kwanza katika somo hilo. Mgogoro huu ulisuluhishwa baada ya Daba kwenda kuonana na mwalimu huyo katika shule ya Sekondari Blazi Dienyi. (Uk. 97).
Ujumbe
Ujumbe ni jumla ya mafunzo tunayoyapata katika kazi ya fasihi baada ya kuisoma au kusikiliza kazi yote. Katika riwaya hii ya “Barua Ndefu kama Hii” ujumbe tunaoupata ni kama ifuatavyo:-
Ukombozi wa mwanamke ni muhimu sana katika jamii. Ukombozi wa mwanamke katika Nyanja zote za maisha ni muhimu kwasababu mwanamke ndiyo chachu ya maendeleo ya jamii kulingana na juhudi alizonazo hasa katika swala la malezi ya familia. Hivyo, mwanamke akikombolewa kijamii, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kifikra jamii nzima itakuwa imekombolewa.
Ili kuleta usawa katika jamii ni lazima wanawake wapewe haki sawa na wanaume katika Nyanja zote za maisha.
Demokrasia ya kweli itapatikana ikiwa mwanamke atapewa haki sawa na mwanaume katika nyazifa mbalimbali za uongozi wa nchi. Kwa mfano, Ubunge au uwaziri
Swala la malezi linahitaji ushirikiano wa wazazi wote wawili na sio kutelekeza jukumu hilo kwa mzazi mmoja tu.
Swala la mapenzi na ndoa lisiingiliwe na dini wala mtu yoyote Yule bali waachiwe wapenzi wenyewe.
Mapenzi ya dhati ni dhana mojawapo ya kuleta umoja, upendo, amani nhivyo kusaidia maendeleo ya Taifa.
Falsafa
Falsafa ni imani aliyonayo mwandishi wa kazi ya fasihi ambayo humfanya kushikiria jambo Fulani. Katika riwaya hii ya “Barua Ndefu kama Hii” mwandishi Mariama Ba. Anaamini katika ufeministi kuwa, mwanamke akipewa haki sawa na mwanamme ndipo ujenzi wa jamii mpya yenye usawa (jamaa) haki, upendo, amani, Demokrasia ya kweli na maendeleo utakuwa umekamilika. Anaamini kuwa kumkomboa mwanamke ni kuikomboa jamii nzima katika unyanyasaji na ukandamizaji.
Msimamo
Msimamo ni ile hali ya mwandishi kusimamia au kushikilia jambo Fulani na kulitetea bila kujali kama jambo hilo linakubalika au la. Katika riwaya hii, mwandishi Mariama Ba. Anamsimamo wa kimapinduzi kwani ameonesha uhitaji wa kumkomboa mwanamke katika Nyanja zote za maisha. Anataka mwanamke apewe haki sawa na mwanamme ili aondokane na ukandamizwaji anaofanywa katika jamii.
Mtazamo
Mtazamo, ni hali ya msanii anavyoyatazama mambo katika ulimwengu wa kifasihi (mazingira aliyonayo mwenyewe). Katika riwaya hii, mwandishi Mariama Ba. Anamtazamo wa kiyakinifu kwa sababu ameweza kuyajadili mambo kwa uwazi bila kuogopa dini au serikali. Ameonesha swala la ndoa za mitaala kuwa ni tatizo bila kuogopa dini ya kiisilamu inayoruhusu swala hilo. Pia ameongelea upendeleo unaofanywa na serikali wa kuwanyima wanawake nafasi za uongozi hasa zile za juu katika utawala bila kuiogopa serikali yake, Hivyo, hii inaonesha kuwa mwandishi anamtazamo wa kiyakinifu.
VIPENGELE VINGINE VYA UCHAMBUZI
Kufaulu kwa mwandishi
Mwandishi amefaulu kifani kwani ameweza kutumia lugha ambayo inaeleweka, pia amefaulu kuteua mandhari ambayo inaendana na wazo lake.
Kimaudhui, mwandishi amefaulu kuliweka bayana wazo kuu bila kuogopa na hivyo ameweza kuifikisha ujumbe wake kwa jamii.
Kutokufaulu kwa mwandishi
Kifani, mwandishi hajafaulu katika uteuzi wa wahusika kwa sababu ametumia wahusika wengine ambao hawakuwa wa muhimu sana. Kwa mfano. Athuman
Kimaudhui, mwandishi hajafaulu kwa sababu amejikita katika kupigania haki za wanawake pekee na kusahau haki za wanyonge wengine kama vile maskini na walemavu.
Jina la kitabu
Jina la kitabu “Barua Ndefu kama Hii” Linasadifu yaliyomo kwani limeweza kuongelea Barua ndefu yenye sura 27 ambayo iliandaliwa kwa rafiki wa mhusika mkuu ambayo inaongelea visa na matukio mbalimbali. Isitoshe ndani ya Barua hiyo kuna barua nyingine ambayo nayo bado inaelezea tukio linaloendana na matukio yaliyomo kwenye barua hiyo(Uk.92).
Vilevile, “Barua Ndefu kama Hii” inasadifu namna ambavyo dhamira mbalimbali hasa dhamira kuu ya ukombozi wa mwanamke ambavyo inaweza kuchukua muda mrefu hadi kufikia hitimisho la ukombozi huo.
B: NADHARIA ZA UCHAMBUZI WA RIWAYA
Dhana ya Nadharia,
Dhana ya nadharia imefafanuliwa na wataalamu mbalimbail.Kwa mujibu wa Wamitila (2003) anaeleza kuwa, Nadharia hutumiwa kumaanisha kauli za kiujumla au kaida zinazomwongoza msomaji katika ufasiri wa maana uliopo katika Fasihi.
Wafula na Njongu (2007) wanafafanua kuwa nadharia ni jumla ya maelezo yanayomsaidia msomaji au mhakiki kuifahamu kazi ya fasihi kwa kufuata utaratibu maalumu.
TUKI, (2004) wanasema Nadharia ni mawazo, maelezo au mwongozo uliopangwa ili kusaidia kueleza, kutatatua au kutekeleza jambo Fulani.
Kwa ujumla naweza kusema kuwa nadhari za uchambuzi wa riwaya ni maelezo yanayomwongoza mhakiki katika kuhakiki riwaya husika. Kwa kutumia Riwaya ya Bara Ndefu Kama Hii iliyoandikwa na Mariama Ba nitaeleza nadharia mbalimbali zilizotumika katika kuichambua riwaya hii kama ifuatavyo:-
Nadharia ya Ufeministi
Kwa mujibu wa Mbatiah (2001) anaelezea nadharia ya ufeministi kuwa ni nadharia inayojishughulish na utetezi wa haki za wanawake dhidi ya ukandamizwaji katika jamii yenye mfumo uliodhibitiwa na wanaume.
Katika riwaya ya “Barua Ndefu kama Hii” Nadharia ya ufeministi imetawala kama nadharia ya uchambuzi ambapo inaonyesha maudhui kubwa ya riwaya hii ni kutetea haki za mwanamke katika Nyanja zote za maisha, yaani kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni. Mfano mzuri unaothibitisha hili ni katika ile sura ya 20. Hivyo, nadharia hii ya Ufeministi imetumika katika riwaya hii kama nadharia ya uchambuzi wa riwaya ikipigania jamii mpya yenye misingi katika amali za kibinadamu wala sio kimaumbile (Jinsia).
Nadharia ya Naratolojia (Simulizi)
Hii ni nadharia ambayo husimulia tukio moja au mengi ya kihalisia au ya kubuni. Katika riwaya hii Nadharia ya Naratolojia imetumika kama nadharia ya uchambuzi wa riwaya hii. Hii inajidhihirisha kutokana na ukweli kwamba, riwaya hii imetumia mtindo wa barua ya kirafiki ambayo inasimulia au kuelezea matukio mbalimbali yaliyompata mhusika mkuu pamoja na jamii yake kwa ujumla. Mfano mzuri wa kudhibitisha nadharia hii ni katika sura ya 13 ambapo mhusika mkuu Ramatulayi anaanza kusimulia mkasa wake.
Nadharia ya kisaikolojia
Hii ni nadharia ambayo huchunguza saikoloija za wahusika kama vile, uzungumzaji wa nafsi, dayolojia ya ndani na ndoto ambazo zinaonesha hali zao za ndani na ambavyo wahusika hao walivyotumia uhusika wao kuibua dhamira mbalimbali katika riwaya. Katika riwaya ya “Barua Ndefu kama Hii” nadharia ya kisaikolojia imetumika ambapo imeonesha muhusika mkuu Ramatulayi alivyoweza kuonesha mawazo yake ya kinafsia. Mfano mzuri unaothibitisha hili ni pale Ramatulayi anaposema;
“Mwanamke anauwezo wa kutambua kabla ya azimio la namna hii” (uk. 88)
Hii inaonesha kwamba kabla ya mhusika kuanza kuzungumza, huanza kuzungumza nafsini. Pia mhusika Dauda Diengi anasema
“Tabia ya kibinadamu…. Mnapogawana keki kila mmoja anataka kipande kikubwa” uk. 83)
Hii inadhihirisha kuwa nadharia ya kisaikolojia imetumika ambapo imeonesha mawazo ya nafsini miongoni mwa wahusika.
Nadharia ya umaksi (kiumaksi)
Nadharia hii hujikita katika kuchunguza historia ya maisha ya binadamu ikielekea katika misingi ya kiyakinifu. Pia kuangalia harakati zinazoendelea katika matabaka ya kiuchumi na kijamii katika ngazi mbalimbai za kifamilia, dini, elimu maadili na utamaduni. Katika riwaya ya Barua ndefu kama Hii” Nadharia ya umaksi pia imetumika ambapo inajidhihirisha kwamba mwanamke ni kiumbe duni ambaye hawezi kuwa katika tabaka la juu (watawala) katika jamii. Hivyo inaonesha kuwa mwanamke ni tabaka la chini ambaye anakandamizwa na kunyongwa haki zake na tabaka la juu ambalo ni wanaume. Mafano mzuri wa uthibitisho wa nadharia hii ni wanawake wahusika katika riwaya hii ambao ni Ramatulayi na Aisatu ambao wilkuwa wanakandamizwa na mfumo wa dini wa ndoa za mitaala, kutokana na maamzi ya waume zao. Kwa hiyo, nadharia hii imetumika kuyachambua matabaka hayo na hatimaye kuhitaji usawa.
Kwa ujumla, hizo ni baadhi ya nadharia ambazo zimetumika katika uchambuzi wa riwaya ya “Barua Ndefu kama Hii”.
C: RIWAYA YA KISWAHILI NA MAPOKEO YA KIASILI
Mapokeo ya Asili katika riwaya ya Kiswahili ni dhana ambayo inatuongoza moja kwa moja katika Riwaya ya majaribio. Riwaya ya majaribio imejadiliwa na wataalamu mbalimbali, kwa mujibu wa Mlokozi; (1996) anafafanua kuwa riwaya ya majaribio ni aina ya riwaya inayojitokeza katika mikondo miwili ambayo hutungwa pasipo kuzingatia kanuni za kawaida za uandishi wa riwaya na mtiririko wa visa na matukio uliozoeleka hukiukwa. Kwa ujumla mapokeo ya kiasili katika riwaya ya Kiswahili (Riwaya ya kimajaribio) ni jumla ya vipengele vya tanzu za fasihi ya kale (Fasihi simulizi) vinavyoingizwa katika riwaya ya Kiswahili.
Kwa kutumia riwaya ya Barua Ndefu Kama Hii iliyoandikwa na Mariama Ba. Vipengele vya mapokeo ya asili (Fasihi simulizi) katika riwaya hii vitajadiliwa kulingana na vilivyojitokeza kama ifuatavyo:-
Miviga, miviga ni taratibu za kijadi ambazo zilifanyika kama sherehe zikiambatana na tukio kubwa la matambiko. Katika riwaya hii, kipengele hiki cha mviga (matambiko) kimejidhihirisha kwanza, mhusika ambaye ni shangazi Nabu ambaye ni mama yake Maudo Ba. Alikwenda kijijini kwao kutambikia ili alipize kisasi cha Maudo kumuoa Aisatu ambaye hakuwa na damu ya kifalme. (uk. 58). Pia mhusika mwingine ambaye ni baba yake Aisatu, alifanya matambiko katika uhunzi wa dhahabu na vyuma ili kuondoa (Djini) Pepo waovu (sura ya 8) vilevile mambo mengine yanayoendana na matambiko ni uganga na ushirikina ulioambatana na utabiri. Huu ulifanywa na malenga - mshirikina. (uk. 109). Hivyo, kipengele hiki kinaonesha mapokeo ya kiasili katika riwaya ya Kiswahili.
Semi, katika riwaya ya “Barua Ndefu kama Hii” mwandishi ametumia semi mbalimbali hasahasa methali, Nahau na Misemo mbalimbali kwa mfano:-
Methali: Mama mwenye mtoto hana muda wa kutalii bali wa kufa nao” (uk. 101)
Misemo: “Ndoa si mnyororo” (uk. 99)
Semi, hizi ni mapokeo ya asili kutoka katika fasihi simulizi ambazo zilitumika kuonya na kuadilisha jamii. Hivyo, haya ni mapokeo ya kiasili katika riwaya ya Kiswahili.
Wahusika, katika riwaya hii ya “Barua Ndefu kama Hii” kipengele cha wahusika kimeonekana kuwa ni kipengele cha mapokeo ya kiasili kwa sababu mwandishi ametumia wahusika ambao ni viumbe wengien kama vile “Safara” (maji yenye uwezo wa kimuujiza) uk 58, “Djini” (Pepo waovu) (sura ya 8) na “Simbi” (Punje za baharini zilizotumika kutabiri”. Haya yote ni majina ya wahusika wa fasihi ya asili (fasihi simulizi) ambayo ni mapokeo ya kiasili katika riwaya ya Kiswahili.
Kwa kuhitimisha, hayo ndiyo mapokeo ya kiasili yanayojitokeza katika riwaya ya Barua Ndefu kama Hii ambayo ni Riwa ya Kiswahili kama ilivyoelezwa hapo juu.
D: ATHARI ZA UTAMADUNI WA NJE KATIKA RIWAYA YA KISWAHILI
Utamaduni wa njie ni jumla ya mitindo yote ya maisha ambayo haikuwepo katika mtindo wa maisha ya jamii ya waswahili hapo awali. Mitindo hiyo imeingizwa katika jamii ya waswahili na hivyo kupelekea riwaya ya Kiswahili kuiga mitindo hiyo.
Utamaduni wa nje umeleta athari kadha wa kadha katika riwaya ya kiswhaili. Kwa kutumia Riwaya ya Barua Ndefu Kama Hii iliyoandikwa na Mariama Ba. Nitajadili athari za utamaduni wa nje katika riwaya ya kiswhaili kama ifuatavyo:-
Atahri katika muundo wa Riwaya utamaduni wa nje umeathiri riwaya za Kiswahili katika upande wa muundo wa riwaya ambapo riwaya za Kiswahili zilifuata muundo wa asili ambao ni muundo msago (moja kwa moja) lakini kutokana na riwaya zenye Utamaduni wa nje ambazo muundo wake huwa ni changamani au rejea, Riwaya ya Kiswahili nayo imeweza kuiga muundo wa namna hiyo. Kwa mfano. Katika riwaya ya “Barua Ndefu kama Hii” mwandishi ametumia muundo wa Rukia (Changamano) ambao haukuwa muundo halisi wa asili wa riwaya ya Kiswahili. Riwaya hii inaanza kuelezea kifo cha mhusuka (Modu) kisha kurejerea matukio kabla ya kifo chake na hatimaye inaonesha maisha. Ya familia ya marehemu baada ya siku za maombolezo. Hivyo muundo huu sio muundo wa asili wa riwaya ya Kiswahili bali ni athari za utamaduni wa nje.
Athari katia suala la maleba utamaduni wa nje umeathiri riwaya ya Kiswahili katika swala zima la maleba ambapo maleba katika riwaya ya Kiswahili yaliendana na utamaduni wa kiafrika kama vile, uvaaji wa mashuka, ngozi za wanyama, njuga na kadhalika. Katika riwaya hii, uvaaji wa Maleba umeathiriwa na utamaduni wa nje kwa kiasi kikubwa ambapo wahusika wake wametumia maleba ya kigeni. Kwa mfano uvaaji wa kanzu ambao umeonekana kwa wahusika kama vile, Imamu (uk. 47), Dauda Diengi (uk. 80-88) nk. Huu ni mtindo wa uvaaji wa waarabu ambao ni watu wa mashariki ya kati. Pia wahusika kama vile; Yasini, Aramu na Diyinaba ambao ni mabinti wa Ramatulayi, wameonekana wakivalia maleba ambayo ni “Suruali” (uk. 103) ambayo ni kinyume na mtindo wa mavazi ya wanawake wa jamii ya waswahili. Mtindo huu ni mtindo wa uvaaji wa utamaduni wa kimagharibi. Hivyo, kutokana na uvaaji huu wa maleba, utamaduni wa nje umeathiri riwaya ya Kiswahili.
Athari katika swala la dini, utamaduni wa nje umeathiri riwaya ya Kiswahili katika swala la dini ambapo riwaya ya Kiswahili ilifuata dini ya asili ambayo ilikuwa ni kuabudu Miungu na mizimu. Katika riwaya hii utamaduni wa nje unaonekana ambavyo umeathiri riwaya ya Kiswahili katika upande wa dini. Tunaona wahusika kama vile, Ramatulayi, Immamu, Daba na wahusika wengine waiamini katika Dini ya kiislamu ambapo wanamuabudu “Allah” Mungu mweza (uk. 48). Dini hii ni dini yenye asili ya utamaduni wa Kiarabu. Hivyo kutokana na suala hili utamaduni wa nje umeathiri riwaya ya Kiswahili.
Kwa kuhitimisha, utamaduni wa nje umeathiri riwaya ya Kiswahili katika mfumo mzima wa maisha ya wahusika ambapo hata vifaa vinavyotumiwa na weahusika hao ni vile vinavyoendana na utamaduni wa nje. Kwa mfano, “eksierei” joko la gesi” pedali” na kadhalika, hivi ni vifaa ambavyo vimetajwa katika riwaya hii ambavyo ni vifaa vya utamaduni wa nje. Hivyo, utamaduni wa nje umeathiri riwaya ya Kiswahili kwa kiwango kikubwa.
MAREJELEO
Madumulla, S. (2009). The Swahili Novel: “Historical Theories and Foundations of Analysis”. Dar- es- salaam. Mture Educational Publishers Ltd.
Mbatiah, M. (2001) Nadharia katika Taaluma ya Kiswahili na Lugha za Kiafrika. Nairobi: Moi Univeristy Press.
Mulokozi, M.M. (1996). An Introduction to Malaysian Swahili. Dar –es- salaam. TUKI.
Utangulizi wa Fasihi. Dar –es- salaam: Chuo kikuu cha Tanzania.
Njogu, K. na Chimera, R. (2007) Ufundishaji wa Fasihi, Nadharia na mbinu. Nairobi: Jomo Kenyaya Foundation.
Senkoro, F.E M.K (2011) Literature and Literature. Dar –es- salaam Kauttu Ltd.
TUKI. (2004) Kamusi ya Kiswahili sanifu. Nairobi: Oxford University Press.
Wamitila, K.W (2003). Dictionary of Literature Teminology and Theory. Nairobi: Focus Publicatiosn Ltd.
Kamsi ya fasihi, Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus Pubication Ltd.
Comments
Post a Comment