RIWAYA YA KISWAHILI NA TAHAKIKI

      RIWAYA YA KISWAHILI NA TAHAKIKI
CHUO KIKUU CHA ARUSHA
NA:  LEBABU S.S




Maana ya Fasihi
Dhana ya fasihi imekuwa ikijadiliwa kwa karne nyingi na wataalamu mbalimbali ulimwenguni kote. Huko Ulaya dhana hii ilikuwa ikihusishwa na vitu kadhaa. Hata Afrika neno fasihi limezua mjadala mkubwa sana kwa wanafasihi katika taaluma hii. Miongoni mwa wataalamu ambao wamechangia kuhusu maana ya fasihi ni pamoja na Sengo na Kiango (1977), Kirumbi (1975), Mazrui (1980) na wengine wengi. Kiulimwengu hasa huko Ulaya dhana ya fasihi imekuwa ikihusishwa na neno la kilatini litera likiwa na maana ya herufi au uandikaji. Hata neno la Kiingereza ‘literature’ limechipuka kutoka hapo. Mitazamo iliyotawala dhana ya fasihi ipo mitano
Mtazamo wa kwanza ni ule unaodai kuwa fasihi ni tafsiri ya neno la Kiingereza Litereture ambalo asili yake ni neno la Kilatini likiwa na maana ya herufi au uandikaji. Hivyo basi mtazamo huu unaamini kuwa fasihi ni jumla ya maaandishi yote katika lugha. Wellek na Warren (1986:20) wanasema Literature as everything in print. Asili ya mtazamo huu ni wa Kimagharibi. 
Wafuasi wa mtazamo huu ni pamoja na Wellek na Warren (1986:20) Sengo na Kiango (1977), Kirumbi (1975), Mazrui (1980) na Mulokozi (1973). Wataalamu kama Sengo, Kiango, Mazrui na Mulokozi waliukubali sana mtazamo huu hasa katika miaka ya 1970 kwa sababu wakati huo taaluma ya fasihi ya Kiswahili ilikuwa katika hatua za mwanzo mwanzo hata dhana yenyewe ya literature ilikuwa bado inatafutiwa istilahi yake ya Kiswahili. Baadaye neno fasihi walipendekeza liwe na maana ya adabu ya lugha na mwishowe neno fasihi lilishinda na kupewa maana ya sanaa ya lugha, bila kujali kama imeandikwa au la, tafsiri inayotumika hadi sasa.
Mtazamo huu ukiutazama kwa makini utakuwa na mapungufu fulani. Kwa mfano
i/. Uwanja wa fasihi wameupanua sana kwani si kila kilichoandikwa ni fasihi
ii/. Fasihi wameinyang’anya kuwa ni mali ya jamii nzima kwani imebagua tu watu wanajua kusoma na kuandika.
iii/. Kama ni hivyo basi chimbuko la fasihi ni ulaya na hapa Afrika hatukuwa na fasihi. Balisdya ametoa rai kuwa fasihi simulizi ambayo ndiyo fasihi ya watu wa chini haikutiliwa maanani.
Mtazamo wa pili ni ule unaodai kuwa Fasihi ni maandishi bora katika jamii bora yenye manufaa ya kudumu Hollis Summers (1989:357) aliposema literature is bells-lettres, a French phrase that means beautiful writing. Dhana hii ya maandishi bora ni marekebisho madogo yaliyofanywa kutoka mtazamo wa kwanza badala ya maandishi yote ikawa maandishi bora ikiwa na maana ya kwamba fasihi ni maandishi bora au kazi ya kisanaa yenye manufaa ya kudumu kutoka katika jamii bora.
Mtazamo huu pia katika dunia ya leo una mapungufu fulani. Unadhani ni mapungufu yapi unayoyaona kutoka katika mtazamo huu?
i/. Pamoja mtazamo huu unatoa uwanja katika kubuni lakini inatoa uzito tu katika maandishi. Na wala hawakufafanua kuwa maandishi bora ni yapi.
ii/ mtazamo huu unaitambua fasihi ni ile iliyoandikwa tu na fasihi simulizi sio fasihi.
iii/Mtazamo wa tatu ni ule unaodai kuwa fasihi ni hisi. Mtazamo huu ulizuka hapa Afrika Mashariki na kuenea sana miaka ya 1970 nao ulidai kuwa fasihi ni hisi ambazo zinajifafanua kwa njia ya lugha. Wafuasi wa mtazamo huu ni pamoja na Ramadhani, J, A katika Mulika 2:6, Balisdya katika Mulika 2:132, Sengo na Kiango katika Hisi Zetu, (1973:2-3). Wafuasi wa mtazamo huu wanaonyesha kuwa mtu anapokuwa na hisi fulani na ili ziwafikie watu lazima zifafanuliwe kwa kutumia lugha. 
Mtazamo huu pia unayo mapungufu yake kwani unachanganya mambo matatu yaani fasihi yenyewe, mambo yanayoelezwa na mtindo au maneno yanayotumika. Kwani Kiango na wenzake wanasema kuwa fasihi huelezea hisi kadhalika mtindo wa kifasihi mara nyingi ni wa kihisia bali fasihi yenyewe si hisi. Maana hii ni sawa na kusema kuwa fasihi huelezea mapenzi lakini fasihi yenyewe si mapenzi.
Mtazamo wa nne ni ule unaodai kuwa fasihi ni tokeo la matumizi ya lugha kwa njia isiyo ya kawaida ili kuleta athari maalum. Mtazamo huu ulianzishwa na wafuasi wa nadharia ya uumbaji (formalism) kutokana na umbo. Waanzilishi wake ni wanaisimu wa Kirusi mwanzoni mwa karne ya 20 akiwepo Roman Jacobson, Viktor Shokhovisk. Kwa mujibu ya watu hawa fasihi hukiuka utaratibu wa matumizi ya kawaida ya lugha katika sarufi, maana na sauti ili kumvutia au kumwaathiri msomaji au msikilizaji. Lugha ya fasihi humfanya msomaji au msikilizaji aitafakari lugha yenyewe badala ya kuutafakari tu ujumbe unaowasilishwa na lugha hiyo. 
Mapungufu ya mtazamo huu yamekosolewa sana na wanafasihi kwani 
i/. mtazamo huu unaelemea mno upande wa fani na kupuuza maudhui, maana na muktadha wa kazi ya fasihi.
ii/. Mtazamo huu unasadifu zaidi ushairi kuliko tanzu zingine za fasihi ambazo si lazima zitumie lugha kwa namna ya pekee.
iii/. Lugha ya fasihi ya namna hii humfanya msomaji au msikilizaji kubaki kujishughulisha na kutafakari mpangilio na ufundi wa maandishi au maneno yalivyotumika badala ya ujumbe wenyewe unaowasilishwa.
Mtazamo wa tano ni ule unaodai kuwa fasihi ni sanaa inayotumia lugha yenye ubunifu bila kujali kuwa imeandikwa au la. Mtazamo huu wa tano hauna siku nyingi, nao umeanza kutumika na kuenea katika karne ya 20. Kwa mujibu wa mtazamo huu hata nyimbo na masimulizi ni fasihi japo hayakuandikwa. Mtazamo huu uliambatana na kuzuka kwa tapo la ulimbwende huko ulaya mwishoni mwa karne ya 18, tapo ambalo liliathiriwa na falsafa za watu kama Kant na Hegel (Eagleton 1983: 20-21)
Mtazamo huu ndio unaotawala hivi sasa katika taaluma ya fasihi ya kiswahili. Inadaiwa kuwa neno fasihi limetokana na neno fasuh, neno la kiarabu lenye maana ya ufasaha au uzuri wa lugha. Hivyo istilahi fasihi katika taaluma ya Kiswahili ina tofauti na istilahi ya literature inayotumika katika Kiingerza. Neno fasihi halihusiani na maandishi wala vitabu bali linahusiana na ufasaha wa kauli (maneno yaliyowasilishwa kwa ufundi fulani). Hivyo basi ieleweke kuwa dhana hii ya fasihi katika Kiswahili inazingatia aina zote za fasihi yaani fasihi simulizi na fasihi andishi.
Kwa kuhitimisha kuhusu fasili ya fasihi tunaweza kusema kuwa fasihi ni tawi la sanaa kama Muziki, ufumaji, uchoraji, ufinyanzi, ususi, uchongaji, maonyesho na utarizi ambayo hutumia lugha kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa hadhira. Labda swali la kujiuliza hapa ni kuwa Sanaa ni kitu gani? Sanaa kwa ufupi sana ni uzuri unaojitokeza katika umbo lililosanifiwa. Kila mwanasanaa huwa na mali ghafi yake ambayo hutumia kuunda sanaa yake. Mfano mchoraji malighafi yake anayoitumia kuchora ni brashi, karatasi, kalamu na rangi. Mtu huyu akitumia mali ghafi zake vibaya kitu atakachokichora hakitakuwa na mvuto au ujumbe alioukusudia kuufikisha kwa jamii hautafika barabara. Hivyo Mwanafasihi mali ghafi yake ni maneno hivyo mtu huyu anapotumia maneno hayo pasipo ufundi ujumbe aliokusudia kuifikia jamii utaifikia kinyume cha alichokitarajia. Fasihi hutumia maneno yawe yameandikwa au yamesemwa ili kutoa picha halisi ya mwanadamu katika maisha yake au uhusiano wake na viumbe wengine, mikinzano yake na mazingira, taabu zake, furaha zake, juhudi zake katika kupiga hatua za kimaendeleo, n.k. Katika ufafanuzi huu tunaona kuwa fasihi simulizi na andishi zimejumuishwa humo kinyume na ufafanuzi wa Kimagharibi ambao huzingatia sana fasihi andishi tu.
Utumiaji wa lugha ya kisanaa ni sifa nyingine ya kuzingatia wakati wa kufafanua dhana ya fasihi. Ili kitu kiitwe fasihi si lazima itumie mkondo wa maandishi bali yaweza kutumia usimuliaji au utendaji. Msanii mzuri wa fasihi ni yule anayeweza kutumia msamiati na miundo ya lugha kwa njia isiyo ya kawaida ili aweza kukamata hadhira yake na kuibua hisi fulani kama hasira, furaha, huzuni, huruma n.k miongoni mwa hadhira hiyo. Matumizi haya ya lugha ndiyo huleta tofauti kati ya lugha ya fasihi na lugha isiyo ya kifasihi.
Chimbuko la Fasihi
Chimbuko la fasihi limeelezwa na wataalamu mbalimbali kwa namna tofauti. Maoni ya wataalamu hawa yanaweza kujumuishwa katika nadharia nne zinazotumiwa kuelezea chimbuko lake.
Nadharia ya kwanza ni nadharia ya kidhanifu: Nadharia hii inadai kuwa chimbuko la fasihi ni Mungu. Nadhari hii ni kongwe sana kwani ilikuwako hata kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Waasisi wa nadharia hii ni wasomi wa kale wa Kiyunani kama vile Hesiod, Plato, Socrate, Aristotle n.k. Wafuasi wa nadharia hii wanaamini kuwa fasihi na sanaa kwa jumla imetokana na Mungu, hivyo msanii huipata ikiwa tayari imeandaliwa na Mungu mwenyewe. Nadharia hii ilipata umaarufu miongoni mwa wayunani wa kale ambao walikuwa na Miungu wa ushairi na muziki waliowaita Muse. Wayunani waliamini kuwa miungu hawa (muse) ndio waliowapa watunzi uwezo na msukumo (muhu au kariba) wa kiroho, kinafsi na kijaziba wa kutunga. Wafuasi wa nadharia hii wanadai kuwa Mungu ndiye msanii mkuu, kaumba ulimwengu kwa usanii mkuu jambo ambalo linadhihirika kutokana na maajabu ya kilimwengu yaliyoumbwa na Mungu. Hata mwanadamu naye pia ni zao la sanaa ya Mungu, hivyo basi mwanadamu alipewa na Mungu kipaji cha kubuni kwani Mungu ndiye msanii mkuu. Kwa mujibu wa nadharia hii, fasihi imekukuwapo tangu kuwapo kwa mwanadamu duniani, haikugunduliwa au kutokea katika kipindi fulani tu cha maendeleo ya maisha ya mwanadamu, bali ni zawadi ya Mungu kwa mwanadamu.
Mawazo haya yaliungwa mkono na Father Nkwera (1976) na Ramadhani katika Mulika 3:5 kwa kusema kuwa fasihi ni sanaa ambayo huanzia kwa Mungu yaani Muumba na humfika mtu katika vipengele mbalimbali. Ni hekima ambayo humshirikisha mtu kumtambua muumba wake. Kwa msimamo huu sanaa haifinyangwi na mtu kwa akili za mtu bali hupokelewa ikiwa tayari toka kwa Mungu.
Mapungufu: 
i/. Dosari ya nadhari hii ni kwamba inachanganya imani na taaluma kwani ni nadharia isiyo na uthibitisho au ushahidi wa kisayansi, hivyo ni ngumu kuijadili kitaaluma.
ii/. Nadharia hii inatafuta chimbuko la vitu vya kitamaduni nje ya maisha ya mwanadamu, nje ya dunia hii, na hivyo kukanusha athari za mazingira na mapambano ya mwanadamu katika kumuumba mtu na utamaduni wake.
iii/. Nadharia hii inamwinua sana msanii kumtoa karibu na jamii alimotoka na kumsogeza karibu na Mungu
Nadharia ya pili ni nadharia ya Sihiri: Nadharia hii inadai kuwa fasihi ni sanaa zilitokana na sihiri. Neno hili linamaanisha nguvu za kimiujiza (magic) inayotumiwa na watu kufanya mambo ambayo sio ya kawaida katika uwezo wa binadamu. Waasisi wa nadharia hii wanadai kuwa fasihi inatokana na juhudi za mwanadamu za kutaka kuuelewa ulimwengu unaomzunguka pamoja na nia ya kutaka kuyatawala mazingira yake. Haja hiyo katika hatua za mwanzo za maendeleo ya mwanadamu haikutimilika ipasavyo kwa kuwa uwezo wa kisayansi na teknolojia ya mwanadamu ya wakati huo ulikuwa bado katika kiwango cha mwanzo. Hivyo sihiri kama nguvu za miujiza ilichukua nafasi ya sayansi na ugunduzi. Wafuasi hawa wanasema kuwa fasihi na sanaa zilichipuka kama vyombo vya sihiri katika kujaribu kuyashinda mazingira. Kwa mfano wawindaji wa mwanzo walichora kwanza picha ya mnyama waliotaka kumwinda siku hiyo kisha wakaichoma picha hiyo mshale wakiamini kuwa kitendo hicho kitatokea kuwa kweli watakapokwenda kuwinda. Nyimbo walizoimba na maneno waliyotumia kufanya sihiri ndiyo ushairi wa mwanzo.
Mapungufu:
i/. Nadharia hii inachanganya dhima na chimbuko. Kutumika kwa fasihi katika sihiri hakuthibitishi kuwa sihiri ndiyo chimbuko lake. Sihiri ni amali moja tu kati ya amali nyingi za wanadamu wa mwanzo zilizotumia sanaa na fasihi.
Nadharia ya tatu ni nadharia ya wigo/uigaji: Nadharia ya wigo ni nadharia ya kale iliyoanzishwa na wataalamu wa Kiyunani ikienezwa zaidi na Plato (republic) na Aristotle (poetics). Watetezi wa nadharia hii wanasema kuwa mwanadamu alianza kuwa mbunifu kwa kuiga maumbile yaliyomzunguka. Hivyo sanaa ya mwanzo zilijaribu kuiga na kusawiri vitu vilivyomo katika mazingira yao kama wanyama, ndege, watu n.k. Plato alihusisha wigo na dhana ya uungu kwa kusema kuwa maumbile na vilivyomo ni wigo tu wa sanaa chasili za kiungu. Hivyo sanaa ya mwanadamu (hasa ushairi) ambayo huiga tu mambo yaliyomo katika maumbile haiwezi kuwa na ukweli au uhalisi kwa kuwa inaiga maumbile ambayo nayo yanaiga kazi ya Mungu. Plato alishauri kupiga marufuku baadhi ya mashairi yaliyokuwa yanapotosha ukweli. Nadharia hii ya wigo ilitawala sana huko ulaya mpaka karne ya karibuni. Katika karne ya 16 mwanafalisafa ya Kiingereza na mhakiki wa kazi za kifasihi Sir Philip Sydney alisema hivi, Ushairi ni sanaa ya wigo kwa maneno mengine ni uwakilishi, ni kunakili sura ya kitu. Ni taswira inayozungumza yenye lengo la kufunza na kuburudisha.
Mapungufu:
i/. Nadharia hii inasisitiza sana uigaji na kusahau suala la ubunifu ambalo ndilo uti wa mgongo katika sanaa na fasihi. Ni kweli kwamba kila sanaa ina chembe fulani ya uigaji lakini sio fasihi yote huiga kwani kama ingekuwa hivyo kila mtu angekuwa msanii. 
Nadharia ya nne ni nadharia ya uyakinifu: Nadharia hii inajikita katika fikra za Marx na Engel. Watu hawa ni Wajerumani waliokuwa wanaishi Urusi na kuanzisha mawazo yaujamaa. Nadharia hii inadai kuwa chimbuko la fasihi ni Mwanadamu. Mwanadamu ni zao la maumbile asilia ya ulimwengu. Mabadiliko ya mwanadamu kutoka katika hali ya unyama (usokwe) kwenda katika hali ya utu yamechukua mamilioni ya miaka, halikuwa tukio la siku au wiki moja tu. Utamaduni ikiwemo lugha na fasihi ni zao la mabadiliko hayo. Watetezi wanafafanua kuwa mwanadamu alianza kubadilika alipoanza kuwa mfanyakazi, akaanza kuzalisha mali na hivyo kubadili mazingira ya kimaumbile aliyoyakuta. Mabadiliko haya yalimfanya agundue kuwa alistahili kuratbu shughuli zake ili aweze kuyadhibiti mazingira yake vizuri zaidi.
Katika uzalishaji huo wa mali ilibidi mwanadamu ashirikiane na wenzake. Marx na Engels waliita kipindi hiki ni ujima. Hivyo alihitaji chombo cha kuwasiliana na kuelewana nao. Lugha ilianza tu kama njia ya kurahisisha mawasiliano hayo. Baadae lugha hiyo ikawa chombo cha sanaa yaani fasihi.
Fasihi hiyo ya zamani ilitumika kama zana za uzalishaji kwa lengo la kuchapua kazi. Aidha, ilitumika kujenga hisia za kijinsia katika mahusiano ya uzazi, ambao ndio uliokuwa msingi wa wa maisha ya jamii ya wakati huo. Kwa kadri maendeleo ya uzalishaji mali yalivyoongezeka na kumpa mwanadamu muda wa ziada wa kujiburudisha na kustarehe kwa njia ya sanaa. Fasihi ilianza kujitenga na kazi za uzalishaji mali, ikawa ni sanaa ya burudani. Au ya shughuli maalum za kijamii kama sherehe, ibada n.k. Huu ukawa mwanzo wa fasihi.
Mapungufu:
Mapungufu ya nadharia hii ni kwamba baadhi ya maelezo yahusuyo mabadiliko ya mwanadamu kutoka katika usokwe kuingia katika utu, na hatua zake za mwanzo za kujenga utamaduni na lugha, bado ni mambo ya kinadharia ambayo hayajathibitishwa kwa ukamilifu japo ushahidi unazidi kukusanywa kila uchao kutokana na ugunduzi wa akiolojia, sayansi za biolojia, kemia n.k. Hata hivyo nadharia ya kiyakinifu inaelekea kukubalika zaidi kitaaluma kuliko nadharia ya kidhanifu na ile ya wigo. 


FASIHI YA KISWAHI NI IPI?
Dhana ya “Fasihi ya Kiswahili’ kama dhana ya “Mswahili” ilizua mjadala mkubwa miongoni mwa wataalamu na wanazuoni mbalimbali mnamo miaka ya 1970- 1990. Kiini cha mgogoro huu kilikuwa ni madai ya baadhi ya watu kuwa kuna njama za kuwameza waswahili, au kukanusha kuwepo kwa “kabila” hilo la Waswahili (Chiraghdin 1974:35-41; Chiraghdin 1974:57-61; Chiraghdin na Mnyampala 1977: viii-xi; Shariff,1988; Sengo 1995). 


FASIHI YA KISWAHILI:
    Kuenea kwa lugha ya Kiswahili katika sehemu mbalimbali za Afrika mashariki na nje ya mipaka yake kumeifanya lugha hii kuwa na fasihi yake au yenyewe kuwa chombo cha fasihi kwa watumiaji wake. Hii imetokea tangu pale ambapo wakoloni waliingia katika ukanda huu wa Afrika ya mashariki; Ikiwa ni miongoni mwa karne ya kumi na tisa (19).
   Hivyo basi kutokana na fasihi hiyo ndio tunaiita “fasihi ya kiswahili”. Wataalamu kama vile Syambo Mazrui (1992) na Atamin M. Mazrui (2016) wamathibitisha hili. Uthibitisho huu umepatikana pia katika kitabu cha Swahili beyond the boundaries (2007).
    Hawa wameona kuwa fasihi ya Kiswahili ni ile ambayo imeandikwa kwa lugha ya Kiswahili tu. Hii yaweza kuwa inazungumzia utamaduni wa Kiswahili au mwingine. Wataalamu hawa wameona kuwa jambo la kuzingatia ni matumizi ya lugha katika uandishi wa kazi hizo au uwasilishaji wake.
    Fasihi hii yaweza kubuniwa na mtu na kuiandika katika lugha ya Kiswahili bila kujali utamaduni wake au asili yake. Hii yaweza kuwa katika mfumo wa Hadithi, Riwaya, Tamthiliya au Ushairi.
Mfano wa fasihi ya Kiswahili ni, Shamba la wanyama yake Kawegere (1967) ikiongelea utamaduni wa kiingereza, Shujaa Okoakwo yake Chinua Achebe ikizungumzia utamaduni wa Nigeria, Habari za mlima yake Ahmed


 FASIHI KWA KISWAHILI:
    Lugha ya Kiswahili baada ya kuwa imeenea katika pande nyingi za ulimwengu imekuwa ikivutia watu wengi katika nyanja tofauti ikiwa ni kuizungumza na hata wengine kuiandika. Kutokana na hayo yote kumezuka fungu la fasihi ngeni katika tasnia nzima ya Kiswahili. 
    Baada ya wataalamu mbalimbali wa lugha kuona umuhimu wa lugha hii kuona kumesababisha hata wataalamu hawa kutafsiri katika lugha ya Kiswahili kazi zingine za fasihi.
Mifano ya kazi hizo ni, Shakeapere, Mabepari wa Venisi (Mfasiri J.K Nyerere 1969) na Bwana Myombokela na Bibi Bugonoka TPH 1980. Hizi ni miongoni mwa kazi zilizotafsiriwa toka lugha za kigeni katika Kiswahili.
    Hivyo basi fasihi kwa Kiswahili ni fasihi iliyotasfiriwa toka katika lugha nyingine yeyote na kuandikwa katika lugha ya Kiswahili. Fasihi hii huenda ikawa inazungumzia tamaduni za waswahili au la, vilevile hata utamaduni wa mtunzi na hata vinginevyo. Maana hii pia imeungwa mkono na Sengo.
FASIHI YA WASWAHILI:
    Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na madai kuwa waswahili hawapo na kama hawapo hata fasihi yao haipo. Senkoro (1976), anaona kuwa waswahili wapo na wamekuwapo kwa miakia mingi.
    Utetezi unaotokea hapa ni kwamba; watu hawa wamekuwepo lakini huenda wamekuwa wakitumia majina mengine kama vile, Wamvita, Waunguja, au Wapemba.
    Ushahidi mwingine ni kuwa watu hawa wamekuwa wakitumia utamaduni mmoja na lugha moja. Hivyo basi ikiwa watu hawa wapo basi hata fasihi yao ipo. Mifano mizuri ni tenzi za Fumo Liyongo na nyimbo mbalimbali za kijamii kama vile nyimbo za sherehe, uvuvi, jando, unyago na shughuli nyinginezo.
    Tunaweza kusema kuwa fasihi ya waswahili ni ile inayotungwa na kufungamana na jamii ya waswahili na utamaduni wao. Kama vile nyimbo za jando, harusi na hata uvuvi.
    Kwa maelezo hayo ni wazi kuwa fasihi ya waswahili ipo kwani watu hawa wamekuwapo toka kale na kwani tunaona hata leo mifano ya tenzi zao.
Mifano ya fasihi hizi ni, Nagona na Mizingire yake Kezilahabi, Rosa Mistika yake Kezilahabi, Nguzo mama yake Penina, Motiki ya ziwa Kimba.


 KABILA LA WASWAHILI:
    Kumekuwa na mjadala mkubwa kwa wataalamu mbalimbali kuhusiana na kuwepo kwa kabila la waswahili. Hii imetokana na kuwepo kwa “fasihi ya Kiswahili” hii imetokea hasa miaka ya 1970 – 1990.
    Kuna wale ambao wamedai kuwa kabila hili halipo na kutaka kuwatowesha waswahili au kukanusha kuwepo kwa kabila la waswahili. Chiraghadin na Mnyapala 1977 pamoja na Shariff 1988, hawa wanadai kuwa waswahili ni watu wa mwambao wa Afrika mashariki na kwamba watu hao wanayo fasihi yao ambayo japo huelezwa kwa lugha ya Kiswahili lakini imekuwa tofauti na ile ya bara. Hivyo kusema kabila la waswahili halipo na kutaka kuwapoka utaifa na utambulisho wao watu hao si sahihi.
    Sengo (1987), yeye hudai kuwa waswahili ni kabila au taifa mahsusi. Hivyo wanayo fasihi yao mahususi ambayo ndiyo inastahili kuitwa “fasihi ya Waswahili”.
    Abdalah Khalid (1977), anadai kuwa waswahili ni watu wa mwambao wa kaskazini kuanzia Barawa (Somalia) hadi Tanga wenyeji wa mwambao wa kusini na visiwa vyake si wahamiaji wa maeneo hayo.
    Pia kuna wale walioona na kukanusha kabisa kuwa hakuna kabila la Waswahili. Wao waliona kuwa; “Tunaamini kuwa kazi ya fasihi ya Kiswahili au la kutokana na jinsi ilivyotambulisha na inavyojihusisha na utamaduni wa waswahili. Hapa neno “Waswahili” halimaanishi kabila la Waswahili kwani kabila la namna hiyo halipo leo (Waswahili hapa ni wananchi wa Afrika mashariki na kati kwa ujumla na wala si wale tu wanaoishi katika pwani ya nchi hizi)”. Senkoro (1988).
    Hivyo basi kwa mtazamo wa kundi, tunaona kuwa ni kweli kwamba kabila hili la waswahili halipo kwani kwa mtazamo wa ndani ni kwamba kabila hili lingekuwepo tungeliona hadi sasa, lakini ni tofauti kabisa kuwa kabila hili halipo miongoni mwa makabila yote ya Afrika Mashariki na kati.

MSWAHILI:
    Dhana ya mswahili ni nani ni dhana pana na imejadiliwa na wataalam mbalimbali. Uwepo wa mjadala huu umetokana na dhana ya mswahili kuwa tata na waso waswahili lakini pia na waswahili wenyewe. Massamba (2002).
    Stigand 1913), anaeleza kuwa Mswahili ametokana na uzao wa mmoja wapo wa waarabu au waarabu na waajemi walioishi katika upwa wa Afrika mashariki.
    Steer (1870), anasema Mswahili ni mtu mwenye mchanganyiko wa kinegro na kiarabu.
    Ponera (1870), Mswahili ni mtu mwenye kiwango kikubwa cha umilisi wa lugha ya Kiswahili. Ni mtu ambaye amefungamana sana na mila na desturi ya jamii ya watu watumiao lugha ya Kiswahili kiasi hata cha kumuathiri kifikra, mtazamo na itikadi.
    Dafina ya Kiswahili wanasema inaoonekana ni vigumu sana kupata mswahili ambaye ni mmiliki wa lugha hii ya Kiswahili. Hivyo msawhili anaweza kutazamwa kwa namna mbalimbali kama ifuatavyo;
    Mswahili; anaweza kuwa ni mtu wa mjini aliyeacha dini, utamaduni, mila na desturi zake za asili na kukimbilia dini, mila na tamaduni za kutoka mataifa mengine kutoka uarabuni na nchi za magharibi.
    Mswahili; anaweza kuwa ni mtu ambaye anazungumza vizuri lugha ya Kiswahili kwa kufuata taratibu zote za kiisimu na utamaduni wa lugha ya Kiswahili.
    Mswahili; anaweza kuwa mkazi wa pwani ya Afrika mashariki.
     Mswahili; anaweza kuwa mtu anayeishi maeneo ya kanda ya mjini(uswahilini)
     Mswahili ni mtu mwenye maumbile ya kiafrika. Ikimaanisha ni mtu mwenye miraba minne.


AINA ZA FASIHI

FASIHI ANDISHI
Fasihi andishi ni ambayo uumbaji, uwasilishaji na uhifadhi wake unategemea maandishi. Fasihi hii inatofautiana na fasihi simulizi ambayo inategemea usimulizi. Katika fasihi andishi fanani anatumisa karatasi na kalamu kuelezea hisia zake au mambo yanayomkera ambayo yanafanyika katika jamii yake.
Chanzo cha Fasihi Andishi
Sanaa ya uandishi ilianza na ilipiga hatua kubwa wakati wa uibukaji wa viwanda na shughuli za biashara. Katika shughuli hizi watu hawakupata muda na mazingira ya kukaa na kusimuliana hadithi kama ilivyokuwa wakati wa ujima na umwinyi. Kwa kuwa watu waliendelelea kuwa na hamu ya kutaka viburudisho na mafunzo kwa njia ya fasihi, basi baadhi ya watu walianza kuandika kazi za fasihi. Waandishi wa awali walianza kunakili kazi za fasihi simulizi. Maandishi mengi ya awali yalikuwa kazi za fasihi simulizi zilizohifadhiwa katika maandishi. Baadaye waandishi waligeuza muundo na kuandika hadithi mpya ambazo hazikuwahi kusimuliwa. Hadithi hizi zilikuwa za kubuni. 
Fasihi andishi ya Kiswahili imechipuka kutokana na tanzu mbalimbali za fasihi simulizi pamoja na fasihi andishi za kigeni. 

 
KUKUA NA KUENEA KWA FASIHI ANDISHI
Kazi nyingi za fasihi andishi zimeathiriwa na fasihi simulizi kifani. Waandishi wengi wanatumia majina ya wanyama (ambayo ni ya fasihi simulizi) katika kazi ya fasihi andishi. Kwa mfano mizimu, Mahoka, na wanyama. Na wengine wameathiriwa kimaudhui kiasi cha kutumia vipera vya fasihi simulizi katika uandishi wao kama kuandika vichwa vya hadithi kwa kutumia methali. 
Kabla ya uhuru waandishi waliathiriwa na ukoloni katika fani na maudhui ya kazi zao. Na baada ya uhuru wakawa makini katika upande wa fani na maudhui. Katika fani kipindi baada ya uhuru vipengele vyote vya matumizi ya lugha, mandhari, mtiririko wa uumbaji wa wahusika umekuwa ukikomaa mfano katika lugha, lugha iliyotumika ilikuwa ni Kiswahili sanifu na ni ya kisanaa zaidi. Mandhari ya kazi zao yalionyesha mazingira halisi ya Tanzania. Kimaudhui migogoro iliyojadiliwa ni ile iliyotokana na matatizo yaliyo katika jamii na ambayo yanaendana na wakati.  Je kipindi hiki cha utandawazi waandishi wameathiriwa kivipi kwa upande wa fani na maudhui?
Matatizo ya Ukuaji na Kuenea kwa Kazi ya Fasihi Andishi
Wewe kama msomi unafikiri ni matatizo yapi yanachangia kutokua na kuenea kwa fasihi andishi nchini?
Uchache wa wataalamu wa waandishi
Ukosefu wa vifaa na fedha
Kiwango cha chini cha maendeleo ya elimu
Tatizo la usambazaji
Uchache wa kazi za fasihi
Soko la ajira
Tanzu za Fasihi Andishi
Zipo tanzu kuu tatu za fasihi andishi na kila utanzu umegawanyika katika vijitanzu (vipera)kama ifuatavyo:
Hadithi Fupi (nonela)
Riwaya (hadithi ndefu)
Drama: Katika drama kuna tamthiliya, vichekesho na ngojera
Ushairi: Katika ushairi kuna mashairi, tenzi na ngojera

RIWAYA

DHANA YA RIWAYA
Riwaya imefasiliwa na wataalamu mbalimbali miongoni mwao nikama vile,
Muhando na Balisidya (1976:62), wanasema riwaya ni kazi ya kubuni, ni hadithi ambayo hutungwa kufuatana na uwezo wa fanani kuibusha mambo kutokana na mazoea au mazingira yake. Wanaendelea kusema kuwa riwaya yaweza kuanzia maneno 35000 hivi na kuendelea.
Encyclopedia Americana (EA), Jz. 20 (1982) wakinukuliwa na Mulokozi (1996) wanasema, riwaya ni hadithi ya kubuni inayotosha kuwa kitabu.
Udhaifu; Maelezo haya yanaibua utata kwani hayafafanui kitabu kinapaswa kuwa na urefu kiasi gani. Mathalani kwa mujibu wa UNESCO katika Mulokozi (1996) kitabu ni chapisho lolote lenye kurasa 48 au zaidi. Ama urefu wa kitabu hautegemei idadi ya kurasa tu pia unategemea ukubwa wa kurasa (upana na kina) ukubwa wa maandishi na mpangilio wake.

Wamitila (2002) Senkoro (2011) hawakubaliani na kigezo cha kufasili riwaya kwa kutumia kigezo cha urefu. Mfano Senkoro anaeleza kuwa, “Ikiwa tutakichukua kipimo cha jumla ya maneno (75,000) kuwa kielelezo cha riwaya basi itaonekana kuwatunariwaya chache mno katika fasihi kwa hali hiinadhani sifa ya mchangamano ni nzuri zaidi kuelezea maana ya riwaya” (uk. 56)
Naye Wamitila anendelea kuelezea kuhusiana na suala urefu kuwa, “Kigezo hiki cha urefu hakifai tunapoziangalia kazi za fasihi ya Kiswahili...Mfano kazi mbili za E. Kezilahabi, “Nagona na Mizingile” hazina idadi kubwa ya maneno lakini ni riwaya”

Mlacha (1989), riwaya ni utungo wa nathari wenye kutongoa hadithi yenye urefu fulani, visa vinavyooana na inayozingatia suala nyeti kwa muda maalumu.
 Kwa mujibu wa Senkoro (2011) riwaya ni kisa ambacho urefu wake unakiruhusu kitambe na kutambaa mahali pengi na kuambaa vizingiti vingi vya maisha kama apendavyo mwandishi wake. Anaendelea kueleza kuwa riwaya ni hadithi ndefu ya kubuni yenye visa vingi, wahusika zaidi ya mmoja na yenye mazungumzo na maelezo yanayozingatia kwa undani na upana maisha ya jamii.
 Wamitila (2003), ameeleza kuwa riwaya ni kazi ya kinathari au bunilizi ambayo huwa na urefu wa kutosha, msuko uliojengeka vizuri, wahusika wengi walioelezwa kwa kina na yenye kuchukua muda mwigi katika maandalizi na huhusisha mandhari maalumu.  

Kwa ujumla riwaya ni hadithi ndefu ya kubuni yenye mawanda mapana, lugha ya kinathari, mchanganyiko wa visa na dhamira, wahusika zaidi ya mmoja na matukio yaliyosukwa kimantiki yenye kufungamana na wakati na kushabihiana na maisha halisi ya mwanadamu. Dhima za riwaya ni sawa na dhima za tanzu zingine za fasihi.:

Riwaya ya Kiswahili ni ile ambayo inafungamana na utamaduni wa jamii ya waswahili katika lugha ya kiswahili ambao hupatikana katika nchi ya Afrika mashariki. Pia ni ile riwaya ambayo inawahusu waswahili wenyewe.


VIPENGELE VYA MSINGI KATIKA RIWAYA;
Inaonyesha kuwa ili kujua maana ya riwaya ni vyema kuzingatia mambo kadhaa ambayo ndiyo ya msingi, na mambo hayo ni;
Lazima riwaya iwe na lugha ya kinathari/masimulizi ya kinathari
Isawiri maisha ya jamii,
Iwe na masimulizi ya kubuni na visa virefu,
Wahusika zaidi ya mmoja,
Iwe na mpangilio na msuko wa matukio,
Riwaya iwe na maneno kuanzia elfu thelathini na tano 
Riwaya ni lazima ifungamane na wakati yaani visa na matukio ni lazima viendane na matukio mbalimbali katika jamii.
Uchangamano wa visa
Tofauti Kati ya hadithi fupi na Riwaya
Kufanana
Ubunifu: Zote ni fani za kubuni. Hubuniwa makusudi kabisa na mtunzi binafsi ambaye huisanifu na kuipanga hadithi yake kwa namna anayotaka.
Msuko: Zote huwa na msuko wa matukio uliopangwa kwa namna yenye kuleta mantiki na mshikamano wa simulio mzima.
Lugha: Zote zinatumia lugha za nathari
Uhalisia: Zote huelemea katika uhalisia. Hujaribu kusawiri ulimwengu kama ulivyo.
Kutofautiana
Urefu: Hadithi fupi ni fupi ambayo haizidi maneno 10000 wakati riwaya ni ndefu inaweza kuzidi maneno 10000
Uchangamano: Hadithi fupi ina muundo sahili usiochangamana yaana una tukio kuu moja wakati riwaya ima muundo changamano kutokana na uwingi wa matukio
Wahusika: Hadithi fupi huwa na wahusika wachache aghalabu mhusika mkuu huwa ni mmoja au wawili. Wahuska hawa hawakui na tabia zao hudhihirika kutokana na matukio wakati riwaya huwa na wahusika wengi. Wahusika wakuu huweza kuwa zaidi ya wawili na wahusika wake hukua na tabia zao hujenga matukio.
Dhamira: Hadithi fupi huwa nadhamira chache aghalabu dhamira kuu moja wakati riwaya huwa na dhamira kuu na dhamira ndogo ndogo nyingi.
Mandhari: Hadithi fupi huwa na mawanda finyu kiwakati kijiografia wakati riwaya huwa na mawanda mapana kiwakati kijiografia.


CHIMBUKO LA RIWAYA
TUKI (2004:48) wanasema chimbuko maana yake ni mwanzo au asili.
Tanzu za asili zinaonesha kuwa ndizo zilichangia kwa kiasi kikubwa sana katika kuibua riwaya za Kiswahili. Na yafuatayo ni mawazo ya wataalamu mbalimbali juu ya chimbuko la riwaya ya Kiswahili.
Madumulla (2009) ameeleza kuwa riwaya ilitokana na nathari bunifu simulizi kama vile hadithi, hekaya, na ngano inayosimuliwa kwa mdomo. Anaendelea kusema kuwa fasihi ilitokana na maandiko ya fani ya ushairi hususani tendi za Kiswahili katika hati za kiarabu kwa sababu ndiyo maandishi yaliyotamba katika Pwani ya Afrika Mashariki. Wazungu na waarabu hawakubadilishana maarifa kwa urahisi na hivyo pakapelekea kuwa na majilio ya taratibu za maandiko ya kinathari. Mwanzoni riwaya zilitafsiriwa kwa Kiswahili toka katika lugha za ulaya na kufanya riwaya za Kiswahili kutokea. Mfano wa riwaa hizo ni kama vile; Habari za Mlima iliyoandikwa na Sheikh Ali Bin Hemed (1980).
Senkoro (2011) anaeleza kuwa riwaya iilizuka kutokana na maendeleo na mageuzi ya kiutamaduni, uchangamano wa maisha ya kijamii, kisiasa, kiuchumi, na kiutamaduni yaliyopelekea haja ya kimaudhui zaidi ya ngano na hadithi fupi. Anaendelea kusema kuwa riwaya za kwanza zilitafsiriwa toka riwaya za kizungu mpaka za kiswahili. Anasema riwaya mojawapo ni ile ya James Mbotela ya Uhuru wa Watumwa. 
Naye Senkoro (2011) anaeleza kuwa riwaya ni utanzu uliozuka kutokana na hali mahususi za kijamii. Riwaya kama ile ya kiingereza ya “Robinson Crusoe” iliyoandikwa na Daniel Defoe ni miongoni mwa riwaya za mwanzo. Anasema riwaya ilizuka kutokana na maendeleo na mageuzi ya kiutamaduni na viwanda. Suala la ukoloni na uvumbuzi pia liliumba hali ambazo zilihitaji kuelezwa kwa mawanda mapana zaidi ya yale ya ngano na hadithi fupi. Kupanuka kwa usomaji hasa wakati wa vipindi vya mapinduzi ya viwanda huko ulaya kulifanya waandishi waandike maandiko marefu kwani wakati huo ndipo walipoibuka wasomaji hasa wanawake waliobaki majumbani wakati waume zao walipokwenda viwandani kufanya kazi.
Mulokozi (2017) anaeleza kuwa chimbuko la riwaya ya Kiswahili lipo katika mambo makuu mawili ambayo; ni fani za kijadi za fasihi pamoja na mazingira ya kijamii.
Fani za kijadi za fasihi, Mulokozi anaeleza kuwa riwaya haikuzuka hivihivi tu bali ilitokana na fani za masimulizi yaani hadithi, na ndipo zikapatwa kuigwa na watunzi wa riwaya wa mwanzo. Fani hizo zilizopata kuchipuza riwaya za mwanzo ni kama vile; riwaya za kingano, tendi, hekaya, visakale, historia, sira, masimulizi ya wasafiri, insha na tafsiri.
Ngano, 
Ngano ni hadithi fupi simulizi za kubuni na nyingi hasa zinawahusu wanyama, wadudu, mimea na viumbe wengine. Lakini zipo pia ngano zinazohusu malaika, binadamu, mazimwi na majini. Mara nyingi ngano huwa na msuko sahihi na wahusika wake ni bapa na wahusika hao ni mchanganyiko wa wanyama, mazimwi na binadamu. Mfano wa riwaya zilizo chukua visa vya kingano ni kama vile riwaya ya Adili na Nduguze ya Shaban Robart (1952), Lila na Fila ya Kiimbila (1966), Kusadikika ya Sharban Robart (1951).
Machapisho ya mwanzo ya nathari katika Kiswahili ni mikusanyo ya ngano iliyoharirirwa na Askofu Edward Steere (1866) Specimens of Swahili (Short Tales”), (UMCA)  Zanzibar; Hadithi za Unguja (1867); na “Swahili Tales as Told by Natives of Zanzibar”  (1970) na baadaye yakafuata machapisho mengine kama vile; Mfalme wa Nyoka na Hadithi Nyingine ya R.K. Watts, Hadithi za Esopo N.K. Dhamira za riwaya za kingano ni kama vile choyo, mgongano kati ya wema na uovu na tamaa.
Hekaya
 Hekaya ni hadithi za kusisimua kuhusu masaibu na matukio ya ajabu yaani yasiyokuwa ya kawaida.  Mara nyingi masaibu hayo hufungamanishwa na mapenzi.  Pia hekaya ni ndefu kiasi yaani sio ndefu kiasi cha kama riwaya. Huko ulaya hekaya zilichangia kuibuka kwa riwaya chuku.  Katika jamii ya waswahili hekaya zilikuwa zimeenea sana kipindi cha kabla ya ukoloni. Mifano ya hekaya ni kama vile; Hekaya za Abunuasi ya C.M.C.A. 1915, Sultan Darai (1884), Kibaraka ya (1896) na hekaya ya Jonson, F. na Brenn, E.W, katika hekaya ya Alfa-Lela-Ulela ya kuanzia 1929. Hizo ndizo baadhi ya hekaya za mwanzo lakini baadaye ziliathili riwaya za Kiswahili kama vile; Hekaya ya Adili na Nduguze ya Sharban Robart (1952), hekaya ya Ueberu Utashindwa ya Kiimbila (1971), na Hekaya ya A.J. Amiri, ya Nahodha Fikirini, (1972).
Tendi (utendi), 
Ni hadithi ya kishairi kuhusu mashujaa wa kihistoria na wa kubuni, ambao waweza kuwa ni wa kijamii au kitaifa. Inayojikita katika matukio makuu yenye kubeba na kuakisi mawanio na mustakabali wa taifa au kundi mahsusi. Kwa kawaida baadhi ya tendi zina sifa za kiriwaya ila tu badala ya kuwa na umbo la kinathari zenyewe zina umbo la kishairi. Kuna tendi za aina mbili ambazo ni tendi andishi na tendi simulizi. Riwaya pevu kama tendi husawiri mawanda mapana ya kijamii na kihistoria. Huwa na wahusika wababe yaani mashujaa wenye kuwakilisha pande zinazopingana. Mfano wa tendi ni kama vile; Utendi wa Vita vya Wadachi Kutamalaki Mrima ya Hemedi Abdallah, (1895), Utendi wa Ras (Ghuli), Utenzi wa Fumo Liyongo wa Mohamed Kijumwa K. (1913) Tendi, katika riwaya za Kiswahili imetumia wahusika watatu ambao ni wahusika wa kubuni, wahusika wa kidini na wale wa kijadi wa Kkiafrika.
Riwaya za kusisimua kama zile za E. Musiba Kikosi cha Kisasi (1979), B. Mtobwa, Tutarudi na Roho Zetu (Heko, 1987), zimetumia sana mbinu za kiutendaji katika msuko wake wa matukio na uteuzi wa wahusika.
Visasili,  
Hizi ni hadithi zinazohusu asili na hatima ya watu, vitu, viumbe, ulimwengu na mataifa, na pia huangalia uhusiano wa wanadamu na mizimwi pamoja na miungu. Hadithi za kivisasili zinapoonyeshwa huaminika kuwa na kweli tupu hasa kwa kusimulia matukio mengi ya kiulimwengu. Hadithi zihusuzo kuumbwa kwa ulimwengu na kuumbwa kwa mwanadamu, mathalan zile za Adam na Hawa ni visasili. Riwaya imekopa baadhi ya dhamira zake, motifu na wahusika kutokana na visasili. Ipo mifano mingi ya riwaya za Kiswahili zilizoathiriwa na visasili
Mfano riwaya ya Lila na Fila ya Kiimbila (1966) ambayo imekopa motifu ya asili ya ziwa Ikimba huko Bukoba. Hadithi ya Mungu wa Kikuyu huko Kenya. Roza Mistika ya Kezilahabi (1971), Nagona (1987) na Mzingile (1991), Siku ya Watenzi Wote ya Sharban Robart n.k.  Mbughuni (1982) ameonesha kuwa baadhi ya wahusika wa kike wa riwaya za Kiswahili wamesawiriwa kwa kuzingatia motifu ya Hawa (mwanamke kama mshawishi wa mwanaume). Motifu hiyo imetokana na kisasili cha wayahudi kuhusu kuumbwa na kuanguka kwa wanadamu wa mwanzo (Adam na Hawa)
Visakale, 
Ni hadithi ya kale kuhusu mashujaa wa taifa, kabila au dini. Mara nyingi visa kale huchanganya historia na masimulizi ya kubuni, na hadithi hizi hupatikana karibu katika kila kabila na kila lugha. Baadhi ya visakale vya Kiswahili ni masimulizi huhusu chimbuko la mij ya pwani, Miji-Kenda na Mwinyi Mkuu huko Zanzibar. Visa kama hivi ndivyo vinavyopelekea kuandikwa kwa riwaya za kliswahili. Mfano wake ni riwaya ya Abdalla Bin Hemed bin Ali Ajjemy (1972) kiitwacho Habari za Wakilindi. Athari ya visakale imejitokeza katika riwaya za M.S. Abdulla hususan Kisima cha Giningi (1968) na ile Hadithi ya Myombekela na Bibi Bugonoka na Ntulanalwo na Buhliwali (1980) ya A. Kitereza.
Masimulizi ya kihistoria, 
Haya ni masimulizi ya matendo ya mwanadamu katika muktadha wa wakati, na ni fani muhimu sana katika jamii yoyote ile. Masimulizi halisi ya kihistoria yaweza kuwa ni ya mdomo au hata maandishi na yote huwa ni chemichemi nzuri ya riwaya. Riwaya nyingi hupata kadhia na visa vyake kutokana na matukio halisi ya kihistoria. Mfano wa riwaya hizo ni; Habari za pate ya Fumo Omari Nabhany (1913). Baadhi yalikuwa ni maandishi ya masimulizi na uchambuzi kwa mfano Habari za Wakilindi. Riwaya zingine zilizoathiriwa na matukio ya kihistoria ni; Uhuru wa Watumwa ya J. Mbotela (1934), Kifo cha Ugenini ya O. Msewa (1977), Kwa Heri Iselamagazi ya B. Mapalala (1992) na Miradi Bubu ya Wazalendo ya G. Ruhumbika (1992).
Sira,
Ni masimulizi ya kweli kuhusu maisha ya mtu au watu. Sira huweza kuwa wasifu yaani habari za maisha ya mtu zikisimuliwa na mtu mwingine au zaweza kuwa tawasifu yaani habari za maisha ya mtu zikisimuliwa na yeye mwenyewe. Sira iliathiri kuchipuka kwa riwaya hasa kwa kuonyesha masilmulizi ya maisha ya mtu toka utotoni mpaka uzeeni. Masimuliza ya riwaya hizi yalikuwa katika masimulizi na hata katika maandishi. Kabla ya ukoloni yalikuwepo mandishi yaliyohusu maisha ya mitume na masahaba.  Mifano ya hadithi hizi ni; Kurwa na Doto ya M. S. Farsy (1960), Rosa Mistika ya Kezilahabi (1971), Kichwa Maji ya Kezilahabi (1974) pamoja na Dunia Uwanja wa Fujo (1975), Mzimu wa Watu wa Kale ya Nkwera (1967), na riwaya ya Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini (1949) na Wasifu wa Siti bint Saad (1958) za Sharban Robart.
Masimulizi ya wasafiri,
Hizi ni habari zinazosimulia masaibu ya wasafiri katika nchi mbalimbali. Hekaya za riwaya chuku za kale zilisaidia kukuza riwaya. Mfano Alfa –Lela –Ulela na hadithi ya Robinson Kruso 1719 ilihusu safari ya baharini ya mhusika mkuu ambaye baadaye merikebu aliyokuwemo ilizama, ndipo akalazimika kuishi peke yake katika kisiwa kidogo. Waswahili ni mabaharia wakubwa na wanazo hadithi nyingi za wasafiri waliovinjari katika bahari ya Hindi kwa malengo mbalimbali. Hadithi hizo bila shaka nazo zilichangia kuibuka kwa bunilizi za riwaya.  Katika fasihi andishi ya Kiswahili tafsiri za Alfu- Lela- Ulela, hususan Safari Saba za Sindbad Baharia zilianza kusomwa tangu karne ya 19. Baadye vilifuata vitabu vilivyo andikwa na Waswahili wenyewe kama Sulemani bin Mwenye Chande (Mwinyichande) na wenzake Safari za Waswahili. Ndipo zikafuata riwaya kama vile; Mwaka katika Minyororo ya Samweli Sehoza (1921), Tulivyoona na Tulivyofanya Uingereza (1932) ya Martin Kayamba, Uhuru wa Watumwa na Kwa Heri Iselamagazi.
Insha,
 Ni maandiko ya kinathari yenye kuelezea, kuchambua au kuarifu kuhusu mada fulani. Zipo insha za aina nyingi kama vile, makala, hotuba, tasnifu, michapo, barua, sira, maelezo n.k. Insha nyingi ni fupi mfano kuanzia maneno kama 500 na 10000 japo zingine zaweza kuwa ni ndefu kiasi cha kuwa tasnifu za kufikia kiwango cha kuwa kitabu. Athari ya insha kwa upande wa riwaya inahusiana na uenezaji wa ufundi wa mazoea ya kuandika kinathari, na mbinu za kupanga hoja kimantiki. Athari ya insha inajitokeza zaidi katika riwaya za fikra na falsafa. Mfano wa vitabu vilivyoathiriwa na insha ni Siku cha Watenzi Wote ya Sharban Robert na Kichwa Maji cha Kezilahabi.
Shajara, 
Ni kitabu cha kumbukumbu za matukio ya kila siku. Mila ya kuandika shajara ilikuwa imekwishaota mizizi huko Ulaya na Asia karne nyingi kabla riwaya haijagunduliwa, hivyo yawezekana kuwa jadi hii iliathiri utunzi wa riwaya hasa zile za kisira. Katika karne ya 19 Nikolai Gogol (1809-1852) aliandika hadithi fupi ya kishajara iitwayo Zapiski Sumasshedshevo (Diary of a Madman) iliyochapishwa 1835. Miongoni mwa hadithi-shajara mashuhuri za karne ya 20 ni ile iliyotungwa na Lu Shun iitwayo Shajara ya Mwendawazimu (1918). Ganizi zote mbili ni hadithi fupi na zinamtumia mhusika mkuu kichaa.
Drama
Maigizo mengi hasa ya tamthiliya yaliathiri sana riwaya hasa kwa upande wa usukaji wa matukio na uchanganyaji wa ubunifu na uhalisia. Mfano ni riwaya nyingi za Charles Dickens zina msuko uliosanifiwa kwa uangalifu kama msuko wa tamthiliya.
 Mulokozi (2017). Anaeleza kuwa, kufikia karne ya 16 fani za kijamii zilikuwa zimekwisha enea na kufahamika katika maeneo mengi, hivyo kulihitajika kuwe na msukumo wa kijamii, kiteknolojia na kiuchuni ili ziweze kuvyanza riwaya. Msukumo huo wa kuendeleza fani za kijadi ulikuwa ni wa aina tatu ambao ni;
Ukuaji mkubwa wa shughuri za kiuchumi huko ulaya. Ukuaji huo ulifungamana na biashara ya baharini ya mashariki ya mbali na kuvumbuliwa kwa mabara mawili ya Amerika na kukua kwa nyenzo za uzalishaji wa viwanda huko uingereza, hasa viwanda vya nguo. Malimbikizo ya ziada yaliyotokana na shughuli hizo yalipanda mbegu ya mapinduzi ya viwanda yaliyotokea karne mbili baadaye. Aidha mabadiliko haya yalizua tabaka jipya la mabwanyenye waliomiliki viwanda na nyenzo nyingine za kuichumi. Tabaka hilo lilihitaji fani mpya za fasihi, lilikuwa na wakati wa ziada wa kujisomea, uwezo wa kifedha wa kujinunulia vitabu na magazeti. Hivyo fani ya riwaya tangu mwanzo ilitawaliwa na ubinafsi uliojidhihirisha kiitikadi. Kwa mfano Robinson Kruso ni riwaya ilyosawiri ulimbikizaji wa mwanzo wa kibepari. Ilimhusisha muhusika asiye staarabika aitwaye Fraiday au Juma (kwa tafsiri ya Kiswahili). Ubinafsi huu ulijitokeza pia katika utungwaji wake na usomwaji wake haikusomwa hadharani bali kila mtu alijisomea mwenyewe chumbani mwake.
Jambo la pili lililowezesha riwaya kutokea ni mageuzi ya kijamii na kisiasa, yaliyofungamana na mabadiliko ya kiuchumi. Mataifa ya ulaya yalianza kujipambanua kiutamaduni na kisiasa yalijitenga na dola takatifu ya kirumi. Mabadiliko hayo yalianza kujenga utamaduni wa kitaifa na mifumo ya elimu iliyo hitaji maandishi katika lugha zao wenyewe. Mfano wa mageuzi ya kijamii na kisiasa iliyofanyika ni kama vile; Misahafu ya dini kama biblia kuanza kutafsiriwa kwa lugha za ulaya, Martin Luther alichapisha Biblia kwa lugha za Kidach- Kijerumani miaka ya 1534. Hivyo basi inaonyesha kuwa kadiri elimu ilivyopanuka na ndivyo wasomaji wa vitabu walivyoongezeka na kufanya kuwepo hadhira kubwa nzuri ya wasomaji na watunzi wa riwaya. 
Jambo la tatu ni ugunduzi wa teknolojia ya upigaji chapa vitabu, yaani kwa kutumia herufi zinazohamishika (movable type). Ugunduzi huu uliofanywa na Johannes Gutenberg huko Ujerumani mwaka 1450 ulirahisisha kazi ya uchapaji vitabu katika nakala nyingi na kuondoa kabisa haja ya kunakili miswada kwa mikono. Bila ugunduzi huo kufanyika haingewezekana kuchapisha riwaya nyingi na kuzieneza kwa bei nafuu. Na mifano ya riwaya hizo ni kama vile; Pamela ya Samwel Richardson (1740).
Kutokana na wataalamu mbalimbali kueleza chimbuko la riwaya ya Kiswahili, inaonekana kuwa, riwaya ni utanzu wa fasihi ambao kuzuka kwake kulifungamana na fani za kijadi pamoja na mazingira ya kijamii. Fani za kijamii kama vile, ngano, visasili, visasuli, visakale, insha na nyinginezo zizosimuliwa bila ya kuandikwa kabla ya karne ya 16, zilichochewa na kupewa mwendelezo baada ya kukua kwa sayansi na teknolojia huko ulaya, hasa baada ya ugunduzi wa mitambo ya kupiga chapa kazi za fasihi.


AINA ZA RIWAYA
Mpaka sasa bado wataalamu wa fasihi hawajakubaliana kuhusu namna ya kuziainisha riwaya. Ubishi uliopo ni kuhusu vigezo vya kutumia kuhusu kuainisha riwaya hizo. Kwani mpaka sasa vigezo wanavyotumia kuainisha riwaya ni pamoja na vigezo vya maudhui, umbo, mtindo, muundo, shabaha, kifani, kihistoria, kiitikadi n.k.
Mulokozi (2017:24) ameainisha riwaya kwa kigezo cha dhima, mtindo na maudhui na kupata aina za riwaya zifuatazo.

Istiara
Istiara ni riwaya ya mafumbo ambayo umbo lake la nje ni ishara au kiwakilishi cha jambo jingine. Kwa mfano riwaya ya Shamba la Wanyama (1945) cha Georg Orwell ni ishara na ubeuzi wa mfumo wa utawala wa udikteta wa kisovieti wa enzi za Stalin. Pia riwaya ya Shaaba Robert, Kusadikika ni istiara kuhusu utawala wa mabavu wa kikoloni. Istira nyingine ni riwaya ya Shinikizo la Mauti cha C. Mahundu, na Mkataa Pema cha A. E Musiba.

Riwaya barua 
Ni riwaya ambayo sehemu yake kubwa husimuliwa kwa njia ya barua wanazoandikiana baadhi ya wahusika. Mfano ni riwaya ya S. Richardson, Pamela imo katika kundi hili. Pia riwaya ngingine inayoingia katika kundi hili ni ile ya Mariama Ba ya Barua Ndefu Kama Hii (1980) 

Riwaya –Chuku 
Riwaya- chuku ni hadithi ya vituko na masibu yasiyokuwa ya kawaida. Mara nyingi masaibu hayo huambatana na mapenzi kati ya wahusika wakuu wawili (mwanamke na mwanamme). Mfano wa riwaya-chuku ni Mashimo ya Mfalme Suleimani (1986) cha H. R. Haggard, Adili na Nduguze cha Shaaban Robert, Ubeberu Utashindwa cha Kiimbila, Janga Sugu la Wazawa cha G. Ruhumbika, Damu na Machozi cha E. Shigongo. N.k  

Riwaya Sira
Ni riwaya ambayo husimulia habari ya maisha ya mhusika au wahusika tangu kuzaliwa kwao hadi kufa kwao, yaani tangu utoto wa hadi uzee wao. Hivyo muundo wa wa riwaya hizi huamuliwa na lengo la riwaya husika na mpangilio wa matukio huwa ni wa kimantiki na wakati. Sira hugawanyika katika sehemu kuu mbili, wasifu na tawasifu. Riwaya ya Wasifu ni ile inayoandikwa na mwandishi kuhusu mtu mwingine mfano ni riwaya ya Wasifu wa Siti Binti Saad ambayo imeandikwa na Shaaba Robert kuhusu maisha ya Siti. Tawasifu ni pale mwandishi anapoandika kuhusu maisha yake mwenyewe mfano Maisha yangu na Baada ya Miaka Hamsini cha Shaaba Robert, Bwana Muyombokere na Bibi Bugonoka na Ntulanalwo na Bulihwali cha A. Kitereza, Dunia Uwanja wa Fujo cha E. Kezilahabi, Miradi Bubu ya Wazalendo ya G. Ruhumbika, Nasikia Sauti ya Mama ya K. Walibora. N.k.

Riwaya- Tendi
Ni riwaya yenye kusawiri matendo ya ushujaa na yenye mawanda mapana kama utendi. Aghalabu riwaya hiyo husawiri masuala mazito ya kijamii yenye kuathiri historian na majaaliwa ya taifa linalohusika. Mfano ni Kwaheri Iselamagazi ya B. Mapalala, Ziraili na Zirani ya W. Mkufya, Miradi Bubu ya Wazalendo ya G. Ruhumbika.

Riwaya- Teti
Ni riwaya inayosimulia vituko na masaibu ya maayari (watu wapuuzi, walaghai, wajanja, n.k) kwa njia inayosisimua na kuchekesha. Aghalabu maayari hao huwa ni watu wanaovutia (si wahusika wawi au waovu) wa tabaka la chini na ni bapa. Matukio ya riwaya hii hayana msuko ulioshikamana vizuri. Shabaha yake mojawapo ni kuziteta na kuzikejeli tabia za tamaka tawala na watu mbalimbali katika jamii. Mfano ni Hekaya za Abuduwas.

Riwaya ya Jusura
Ni riwaya inayosimulia masaibu au mikasa yenye kusisimua damu ambayo mtu huweza kukutana nayo wakati wa kutekeleza jambo fulani, kwa mfano awapo safarini, vitani, au katika shughuli ya uzalishaji mali kama uvuvi na uwindaji. Mfano ni Tutarudi na Roho Zetucha B. Mtobwa, E. Musiba Kikosi cha Kisasi, Adili na Nduguze cha Shaaba Robert, E. Semzaba Marimba ya Majaliwa, M.M Mulokozi Moto wa Mianzi. Dhima kuu ya riwaya hii ni kuburudisha, kuelimisha na kujenga moyo wa ushujaa na uzalendo.

Riwaya ya Kifalsafa
Riwaya ya kifalsafa ni hadithi ya fikra na tafakuri; hutafakari na kudadavua masuala makuu kuhusu, ulimwengu, maisha, mauti, na kuwako kwa mwanadamu. Katika fasihi ya Kiswahili mwanzilisho wa riwaya hizi ni Shaaban Robert na baadae E. Kezilahabi katika riwaya zake za Dunia Uwanja wa Fujo, Kichwamaji na baadhi ya riwayya za ubaadausasa na uhalisia mazingaombwe kama Nagona na Mzingile za E. Kezilahabi, Babu Alipofufuka cha S. A Mohamed, Bin- Adam cha K. W Wamitila Ziraili na Zirani za Mkufya n.k.

Riwaya ya Kifanyakazi
Ni riwaya iliyoibuka karne ya 19 huko ulaya na marekani. Ilijikita katika harakati za tabaka la wafanyakazi wa ujira za kudai haki, hali nzuri ya maisha na mfumo bora zaidi wa kijamii. Riwaya za mwanzo za kifanyakazi zilijinasibisha na itikadi za ki-max na zilijaribu kuonesha migongano na mikinzano iliyomo katika mfumo wa kibepari na dhima ya tabaka la wafanya kazi kama mkunga wa kuzalisha mfumo wa kisosholisti usiokuwa na matabaka. Maya nyingi riwaya za kifanyakazi huonesha mapambano ya wazalishaji dhidi ya wenye mitaji (mabepari) na dola yao kandamizi, na kubashiri ushindi wa wafanya kazi na kuasisiwa kwa mfumo mpya usio na matabaka na wenye kutoa haki kwa wote. mfano wa riwaya za kifanyakazi ni Kabwela ya .A J.Jaffari, Kuli ya A. Shafi, Dunia Mti Mkavu ya S.A Mohamed na Walenisi ya K.Mkaangi.

 Riwaya ya Kihistoria
Hii ni riwaya yenye kuchanganya historia halisi na sanaa makusudi ili kutoa maudhui flani. Aghalabu riwaya hii hujikita kwenye matukio makuu ya kihistoria yaliyoathiri mwenendo na mwelekeo wa jamiiau taifa lililohusika. Riwaya ya kihistoria huchanganya wahusika wa historia na wa kubuni, na matukio ya kweli na kubuni. Riwaya hii pia huzingaria zaidi namna matukio makuu ya kihistoria yalivyomuathiri na yalivyoathiriwa na matendo ya mtu binzfsialiyeshiriki. Mfano ni Uhuru wa Watumwa chaJ.Mbotela, Kifo cha Ugenini cha O. Msewa, A. Shafi Kuli, Kwaheri Iselamagazi, Miradi Bubu ya Wazalendo, Haini, Kaburi Bila Msalaba n.k.

Riwaya ya Kijamii
Ni riwaya inayosawiri maisha na matatizo ya kawaida ya kijamii. Matatizo hayo huweza kuwa ya kifamilia, kimahusiano, kitabaka, kisiasa, kitamaduni n.k. utanzu huu ndio wenye idadi kubwa sana ya riwaya Mifano ya riwaya hizi ni pamoja na Kurwa na Doto (M.S. Farsi), Dunia Uwanja wa Fujo, (E.Kezilahabi), Mzishi wa Baba ana Radhi (F. Nkwera), Bwana Myombekere na Bibi Bugonoka (A.Kitereza) na Harusi (A.J. Saffari), Wema na Albino (2008) cha Mkufya, n.k.

Riwaya ya Kingano
Ni riwya yenye umbo na mtindo wa ngano, mathalan huweza kuwa na wahusika wanyama, visa vya ajabu ajabu, mandhari ya kubuni na visa vyenye kutendeka nje ya wakati wa kihistoria. Mifano ni riwaya ya Adili na Nduguze, Lila na Fila, Matatu ya Thamani na riwaya za uhalisia mazingaombwe za Kezilahabi n.k.

Riwaya Kisaikolojia
Ni riwaya inayochimba nafsi ya mhusika ili kudhihirisha fikra, hisia, mawazo, imani, hofu, mashaka, matumaini na matamanio yake binafsi na athari ya mambo hayo kwake binafsi na labda kwa jamii yake mfano wa riwaya hizo ni Kichwamaji E. Kezilahabi, Tata za Asumin S. A. Mohamed, Kiu, M. S Mohamed na Mhanga Nafsi Yangu.

Riwaya ya Mahaba
Ni riwaya yenye kusawiri mahusiano ya kimapenzi kati ya mvulana na msichana, mwanamke na mwanaume. Siku hizi zipo riwaya zenye kusawiri mapenzi haramu (ushoga) kati ya mwanaume na mwanaume au mwanamke na mwanamke. Mifano ni Mwisho wa Mapenzi (1972J. Simbamwene) na Kweli Unanipenda, Jeraha la Moyo ya S, D. Kiango.n.k.

Riwaya ya Ufungwa
Hii ni riwaya inayosawiri maisha na masaiabu ya kifungoni au gerezani. Mhusika mfungwa anaweza kuwa ni mateka wa vita, mhalifu aliyehukumiwa kifungo, mtuhumiwa aliyeko rumande au raia tu aliyewekwa kizuizini kwa sababu za kisiasa au nyinginezo. Riwaya za ufungwa katika fasihi ya Kiswahili ni chache kutokana na wafungwa kutokuwa na tabia ya ya wafungwa ya kutosoma na kuandika wawapo gerezani. Baadhi ya simulizi za kweli katika kundi hili ni Mwaka Katika Minyororo (S. Sehozai 1921), Mau Mau Kizuizini (J.M Kairuki 1965), Miaka 50 Katika Jela (M.N Karanja 1993). Pia zipo hadithi kama Salam Kutoka Jela (M. Abeid 1992), Hisia Kali (N. Justin 1998), Haini (S.A Shafi 2003) na Kizuizini (J. Muthee 2006). 

Riwaya ya Uhalifu
Ni riwaya zinazosimulia vituko vya kihalifu kama wizi, ujambazi, uuaji, magendo, utapeli, na kadhalika. Aghalabu polisi huhusishwa katika kuwasaka na kuwadhibiti wahalifu hao. Mifano ni Kwa Sababu ya Pesa (J. Simbamwene 1972), Buriani (F. Katalambula 1975), Mtu Mwenye Miwani Meusi (L. O Omolo 1970), Ufunguo wa Bandia (H. Rajab1979) n.k.

Riwaya ya Ujasusi
Hii ni riwaya ya upelelezi wa kimataifa. Wajasusi ni wapelelezi wanaotumwa na; serikali, nchi au waajiri wao kwenda nchi nyingine kuchunguza sir zaoa, hasa siri za kijeshi (silaha walizo nazo) siri za kisayansina kiuchumi, ili taarifa hizo ziwanufaishe wao. Wakati mwingine majasusi hutumwa kwenda kuharibu silaha au nyenzo za uchumi za maadui. Mifano ya riwaya hizo ni Mpango (K.M. Kassam1982), Kikosi Cha Kisasi (E. Musiba 1979) na Njama 191981, Roho Mkononi (H. Rajab 1984) na Tutarudi na Rohio Zetu (B. Mtobwa 1987). Katika riwaya hizo ujasusi unafanywa na au dhidi ya nchi ambazo waandishi wanaziona kuwa maadui wa nchi za Kiafrika.

Riwaya ya Upelelezi
Hii ni riwaya ya upelelezi ndani ya nchi husika. Kwa kawaida riwaya hii huwa na vitu viwili; kosa au uhalifu na upelelezi wa uhalifu huo hadi mhalifu anapopatikana. Hivyo wahusika wake huwa ni wahalifu, wadhulumiwa na wapelelezi wakiwamo polisi. Mkondo huu wa riwaya ulianzia huko marekani mwaka 1841 na baadae ulienea duniai kote. Mifano ya riwaya hizi katika fasihi ya Kiswahili ni Mzimu wa watu wa Kale (M.S Abdulla1960), Kisima cha Giningi (Evans 1968), Duniani Kuna Watu (1973), Siri ya Sifuri (1974), Mwana wa Yungi Hulewa (1976), na Kosa la Bwana Msa 1984).
Riwaya ya Utumwa/ Simulizi za Watumwa
Hizi ni ni simulizi zinazohusu watumwa. Simulizi hizi zilitokana na biashara ya utumwa iliyofanyika tangu karne ya 18. Katika fasihi ya Kiswahili kwa bahati mbaya hatuna simulizi nyingi zilizochapishwa, maana watumwa walio wengi hawakupata fursa ya kujifunza kusoma na kuandika kwani ilikuwa kosa la jinai kumfundisha mfungwa stadi hizo (Lodhi 1973). Simulizi chache zilizopo ni zile zilizonukuliwa na wamisionari wa Kizungu kwa kuwahoji watumwa (rej. Wright 1993). Zipo pia simulizi zilizoandikwa na watumwa wenyewe au vizalia wao au zile za kubuni. Mifano ni J. Mbotela Uhuru wa Watumwa 1934, J.R. Nguluma Chuki ya Kutawaliwa 1980, B. Mapalala Kwa Heri Iselamagazi 1992.

Riwaya ya Vita
 Hizi ni bunilizi zinazosimulia kuhusu vita. Riwaya hizi hupendwa kutokana na msisimko na taharuki yake. Riwaya nyingi za vita vilevile ni za kihistoria kwa kuwa vita na historia ni mambo yanayofungamana. Mifano ya riwaya hizo ni M. Kareithi Kaburi Bila Msalaba 1969 inayohusu vita vya Mau Mau nchini Kenya, J.K Kiimbila Ubeberu Utashindwa 1971 inayohusu vita vya ukombozi wa Msumbiji, P. Ngare Kikulacha Ki Nguoni Mwako 1975 inayohusu Mau Mau nchini Kenya, F. Senkoro Uzalendo 1978, J. Mnyune Pigo 1979, K. Chande Mnuko wa Damu 1982 na B. Mtobwa Zawadi ya Ushidi 1987 kinachohusu vita vya Kagera. Hata hivyo katika baadhi ya riwaya hizo vita ni muktadha tu wa kutolea maudhui mengine kuhusu maisha, mahusiano na dhana kuu za kijamii kama vile mauti, mapenzi, usaliti, uzalendo na ukombozi.

 Riwaya ya Vitisho
Ni riwaya yenye visa vya kutisha na kusisimua damu. Aghalabu visa hivyo huambatana na matukio ya ajabu au miujiza. Katika fasihi ya Kiswahili riwaya zenye kushabihiana lau kidogo na uatanzu huu ni zile za kichawi kama vile, N.J. Kuboja Mbogo Simba-Mtu 1971, H.G.M. Mbelwa Mfu Aliyefufuka 1974, C. Mung’ong’o Mirathi ya Hatari 1977, G. Ruhumbika Janga Sugu la Wazawa 2002 na baadhi ya riwaya zinazosawiri mauaji ya kikatili ya Albino kwa sababu za kishirikina.

 Riwaya ya Watoto na Vijalugha
Mtoto ni mtu mwenye umri usiozidi miaka 18. Kijalugha ni kijana wa kike au wa kiume mwenye umri wa kubalehe au kuvuja ungo yaani miaka 12-21. Hivyo riwaya ya hizi ni zile riwaya zinazoandikwa ili kukidhi mahitaji na mapendeleo ya makudi haya mawili ambayo huwa yana umuhimu mkubwa katika jamii yoyote. Riwaya hizi hutofautiana na riwaya za watu wazima katika mambo yafuatayo
Hutumia wahusika wakuu watoto/ vijalugha
Huwa na muundo sahili
Huwa na msuko wenye kujenga taharuki
Huwa na visa vichache lakini vyenye kusisimua
Huepuka kusawri matukio hasi kama ya mauaji, uhalifu mkubwa, uzinzi na uasherati, ngono za waziwazi, n.k. 
Hutumia lugha iliyochujwa na kusahisishwa kulingana na ngazi ya wasomaji waliokusudiwa, lugha hiyo huwa na maneno mepesi na sentensi fupifupi.
Huwa na michoro na picha nyingi 
Hutumia mandhayi yanayo fahamika au kuvutia kwa watoto
Kwa kawaida huwa ni fupi (kurasa 24-48 kwa watoto na 36-150 kwa vijalugha); hata hivyo zipo riwaya chache za vijalugha zenye urefu wa kurasa hata 300 na kuzidi
Hutumia sana fantasia
Huelemea kwenye ramsa (mwisho mwema) kuliko tanzia
Maadishi hutumia fonti kubwa (aghalabu 14 au zaidi) 
Mifano ya baadhi ya riwya hizo ni P. Shija Mashujaa wa Kazakamba 1978 na Vijana Jasiri 1980, E. Lema Safari ya Prospa 1997, B. Mtobwa Kipofu Mwenye Miwani Myeusi 1997, E. Semzaba Marimba ya Majaliwa 2008, S. Ryanga Dogo Munje 2008, n.k.

Saifa: riwaya ya kisayansi 
Neno Saifa ni istilahi inayotokana na utohozi wa neno la Kiingereza “Sci-Fi”, ambaloni kifupi cha “science fiction”, yaani bunilizi ya kisayansi. Riwaya ya kisayansi ni hadithi inayojikita katika taaluma ya sayansi, wakati mwingine ikichanganyika na fantasia na sayansi ya jamii kama msingi wa matukio, masaibu na maudhui yake. Saifa hufanya mambo yenye uwezekano wa kutokea yatokee. Mathalan baadhi ya Saifa hubashiri namna sayansi itakavyoathiri maendeleo ya mwanadamu karne zijazo, na baadhi huonesha namna sayansi inavyoweza kuleta hasara kwa mwanadamu kama ikitumika vibaya bila kuzingatia itikeli (ethics), uadilifu au ubinadamu. Katika fasihi ya kiwsahili bado hawajajitokeza watunzi wa riwaya ya kisayansi halisi, riwaya za E. Kezilahabi, S.A. Mohamed na Wamitila huweza kuchukuliwa kuwa aina ya saifa –fantasia

Riwaya ya Majaribio
 Riwaya ya majaribi hujitokeza katika mikondo miwili. Mkondo wa kwanza ni riwaya ya “mjadala-nafsi”. Mkondo wa pili ni riwaya kweli.
Riwaya ya mjadala nafsi ni aina ya riwaya ya kisasa/ubaadasasa. Hutungwa bila kuzingatia kanuni za kawaida za uandishi wa riwaya. Watunzi wa riwaya hii hudai kuwa umbo la kawaida la riwaya halitoshelezi mahitaji ya zama hizi – halitoshi kuwasilisha kweli kamili ya maisha katika sura zake zote. Mathalan ni vigumu kuelezea mtiririko wa mawazo na hisia zilizomo katika ubongo wa mtu kwa njia za kawaida za uandishi. Hivyo wakabuni njia ya kuelezea mtiririko wa fikra, hisia, na tajiriba ya nafsi ambayo waliita “stream of consciousness.” Katika mbinu hii kanuni za kawaida za sarufi ya lugha na muundo wa riwaya huvunjwa ili kusawiri ulimwengu wa ndani wa mhusika kama unavyojidhihirisha katika fikra, maono na hisia zake. Mifano ya riwaya hizi ni zile za E. Kezilahabi Nagona na Mzingile.

Riwaya-kweli 
Ni riwaya inayotumia mbinu za sayansi ya jamii, mathalan mbinu za uandihi wa habari, historia na sosholojia, ili kusawiri kuelezea maudhui yake. Riwaya hizo husawiri matukio ya kweli kwa kutumia ripoti za magazeti, maelezo ya watu walioshuhudia matukio hayo, takwimu, n.k.    

HISTORIA NA MAENDELEO YA RIWAYA 
Chimbuko la riwaya duniani limeelezwa la wataalam kuwa limetokana na mambo makuu mawili: kwanza ni fani za kijaji za kifasihi, na pili ni mazingira ya kijamii.  Mulokozi (2017) anaeleza kuwa fani za kifasihi ambazo zingeweza kuvyanza riwaya zilikuwepo hapa Afrika Mashariki hata kabla ya ujio wa wakoloni. Kitu ambacho hakikuwepo ni mazingira ya kijamii hususani hadhira kubwa ya watu wajuao kusoma na kuandika, wenye uwezo wa kununua vitabu na wakati wa kutosha kuvisoma; mitambo ya kupigia chapa na mfumo wa usambazaji. Hivyo riwaya ya Kiswahili ilibidi isubiri majilio ya wageni kabla ya kuchipuka. 
Ukoloni ulisaidia kuweka mazingira ambayo yangeweza kuileta riwaya, lakini riwaya yenyewe ilibidi iandikwe na kusomwa na wenyeji kutokana na ujuzi na uzoefu wao. Ili kutimiza azma hiyo watunzi wa riwaya ya mwanzo walirejelea fani za jadi walizozizoea walipata baadhi ya mbinu na maudhui yao, na pengine hata kariha kutokana na fani hizo. Hivyo historia na mendeleo ya riwaya ya Kiswahili tutaingalia katika vipindi tofauti.


Riwaya ya Kiswahili Kabla ya Ukoloni
Kabla ya ukoloni, sehemu kubwa ya fasihi andishi ya kimasimulizi ya Kiswahili ilikuwa ni tendi. Baadhi ya tendi hizo ni kama Kisa cha Anzaruni au Siri Asirari (Binti Lemba 1663), Kadhi Kassim bin Jaffar (Hemed Abdallah, karne ya 19) zilitumia mbinu za kiriwaya, kwa mfano ubunifu wa vituko na msuko wa matukio. Hivyo kwa kiwango hicho tendi hizo ziliandaa mazingira ya kisanaa yaliyo saidia kuzuka kwa riwaya wakati ulipotimu.
Jambo jingine lililosaidia kuchipuza riwaya ya Kiswahili ni tafsiri. Tafsiri za mwanzo katika lugha ya Kiswahili zilikuwa za dini. Tafsiri ya mwanzo iliyofahamika ni ya Sayyid Aidaru bin Athumani iitwayo Kaswida ya Hamziyya (1652). Utendi huo unaomsifia Mtume Muhammad, ulitokana na utendi wa kiarabu uitwao al- Hamziyyah uliotungwa na mshairi wa misri aitwaye Sharafad Muhammad bin Said Al- Bushiri katika karne ya 13. Baada ya Hamziyya kazi nyingi nyingine za kiarabu zilitafsiriwa au kusimuliwa upya kwa Kiswahili. Mfano Utenzi wa Ras Ghuli, Hekaya za Abunuwas na Alfu-Lela- Ulela. Wazungu nao walipoingia walianza kutafsiri vitabu vya biblia kwa Kiswahili; tafsiri za mwanzo kabisa ni Agano jipya na baadhi ya sura za Agano la Kale zilizofanywa na Ludwig Kraft kati ya 1846 na 1848.


Riwaya Wakati wa Ukoloni
Kazi za fasihi ya kizungu zilianza kutafsiriwa kwa Kiswahili kuanzia mwishoni mwa karne ya 19 (kama vile C. Kingsley Mashujaa, hadithi za Wayunani 1889). Pia zilitafsiriwa kazi nyingi zaidi za kigeni, mathalan: H.R. Haggard Mchawi kilichotafsiriwa na M.M.B UMCA1900);  Nael  Nyumba ya Aptonga (The farm of Aptonga na S.P.C.K, London 1924); Safari za Msafiri (Pilgrim’s Progress na S.P.C.K, London 1925); F. Jonson na E. W, Brenn Alfu –Lela- Ulela, London 1928). Hekaya za Abunuwas (S. Chiponde Macmillan 1929) (R.L. Stevenson, Kisiwa Chenye Hazina cha F. Jonson, London 1929); R. Haggard Mashimo ya Mfalme Sulemani na E.W. Brenn na F. Jonson. na D. Defoe Robinson Kruso na Kisiwa chake na EALB km 1962) n.k. Kazi nyingine muhimu zilizotafsiriwa ni baadhi ya tamthiliya za William Shakespear kama. Mfanyabiashara wa Venisi katika mtindo wa nathari. Kazi hizi, pamoja na fani nyingine zilizoigwa kutoka Ulaya, ziliathiri riwaya ya Kiswahili kwani wasomi wengi walizisoma na hata kuziiga.
Mbali na tafsiri kulikuwa pia na maandiko ya mwanzo ya kinathari ya Waswahili wenyewe, hususan maandishi ya tarikhi za miji mbalimbali, mfano Safari za Waswahili, Maisha ya Hemed bin Muhammed (Tippu Tip kwa maneno yake mwenyewe), na Habari za Wakilindi, maandishi haya yaliweka msingi wa mikondo na mitindo ambayo ilifuatwa na watunzi wa baadaye wa riwaya ya Kiswahili.
Mwaka 1930 ilinzishwa Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki. Kamati hii ilihimiza uandishi katika lugha ya Kiswahili kwa njia ya mashindano. Kutokana na mashindano hayo, riwaya ya kwanza ya Kiswahili, Uhuru wa Watumwa (James Mbotela 1885-1976), ilichapishwa mwaka 1934. Baadhi ya riwaya zilizotoka baadaye ni Mzimu wa Watu wa Kale (EALB 1960) cha M.S. Abdulla, Faraji Katalambula Simu ya Kifo (EALB 1965).
Miaka kadhaa baadae baada ya Uhuru wa Watumwa kazi za Shaaban Robert zilitawala (1909-1962). Riwaya yake ya kwanza ilikuwa ni Utubora Mkulima (Nelson 1968) yasemekana ilitungwa mwaka 1946, lakini haikuchapishwa hadi mwaka 1968. Riwaya iliyofuata ni Kufikirika (OUP 1968) iliyoandikwa mwaka 1947, na kuchapishwa mwaka 1967. Riwaya ya tatu, ni Kusadikika (Nelson 1951) ilichapishwa 1951, na riwaya ya nne ni Adili na Nduguze (Macmillan 1952) na kuchapishwa mwaka 1952. Riwaya yake ya mwisho ni Siku ya Watenzi Wote (Nelson 1968) iliandikwa mwaka 1960-62 na kuchapishwa maka 1968. Karibu riwaya zote za Shaaba Robert ziliathiriwa sana na ngano na hekaya, hasa katika muundo wake na uchoraji wa wahusika, karibu wahusika wake wakuu wote ni bapa. Shirika la Vitabu la Afrika Mashariki (EALB) lilianzishwa mwaka 1948 ili kushughulikia uchapishaji wa vitabu kwa lugha za wenyeji. Shirika hilo lilipewa mhuri wa uthibiti wa maandiko (impimature), na kati ya 1948 na 1960 lilichapisha karibu vitabu tofautitofauti elfu moja katika lugha 16 kwa ajili ya shule na wasomaji wa kawaida. Miongoni mwa vitabu hivyo, zilikuwepo hadithi, hasa za kingano, hekaya, na visa. Riwaya za Kiswahili zilizopevuka zilianza kuchapishwa miaka kumi baadaye. Mfano riwaya ya Farsy Kurwa na Doto (EALB 1960). N.K


Riwaya Baada ya Uhuru
Kihistoria, barani Afrika masuala makuu ya kipindi cha baada ya ukoloni kuanzia miaka ya 1960, yalikuwa ukombozi wa bara la Afrika na ujenzi wa jamii mpya baada ya ukombozi wa kisiasa. Masuala haya makuu yalijitokeza katika riwaya ya Kiswahili ya wakati huo. Hivyo palitokea riwaya za kisiasa na kifalsafa zilizo jadili maisha, utawala na ujenzi wa jamii mpya. Riwaya hizo zilizosuta ukandamizaji na ubinafsi, ziliuhakiki unyama wa maisha ya kimji, na zilijaribu kuielekeza jamii katika mkondo wa ubinadamu, usawa na ustawi. Baadhi ya riwaya hizo ni Shaaban Robert Utubora Mkulima, na Siku ya Watenzi Wote. Kwa upande wa ukombozi ni riwaya ya Kiimbila Lila na Fila (Longman 1966), Kaburi bila Msalaba, na Ubeberu Utashindwa.
Kundi linguine la riwaya za wakati huu ni riwaya sisimuzi. (riwaya – pendwa). Matawi mawili ya riwaya hiyo ni Upelelezi na Uhalifu. Riwaya ya upelelezi iliwakilishwa na riwaya ya Mzimu wa Watu wa Kale na Kisima cha Giningi ya Evans 1968, Simu ya Kifo ya Katalambula EALB 1965. Kwa upande wa riwaya ya kihalifu iliwakilishwa na riwaya ya Mtaka yote Hukosa yote ya L.O. Omolo Longman 1968 na Tatizo la Kisauni ya Chadhooro S.J EAPH 1969. Pia kulikuwa na riwaya ya tabia na maadili iliyoandikwa na J.S Somba Kuishi Kwingi Kuona Mengi. EALB 1968 na Alipanda Upepo Akavuna Tufani Heinemann, 1969. Vilevile kulikuwa na riwya ya mila na kiutamaduni, iliyowakilishwa na riwaya ya Kurwa na Doto na F. Nkwera Mzishi wa Baba Ana Radhi EALB, 1968.
Riwaya ya Kiswahili imepevuka na kupanuka zaidi miaka ya 1970-2015. Mambo makuu yaliyoipambanua riwaya ya Kiswahili katika kipindi hiki ni 
Kwanza, ni kutokea kwa watunzi wapya, vijana ambao wameipa uhai mpya riwaya. Baadhi ya watunzi hao ni Euphrase Kezilahabi, 1944, Said Ahmed Mohamed Khamisi 1947, Shafi Adam Shafi, 1940. M. S Mohamed 1943, KGC. Mkangi1944, Z. Burha 1937, A.J. Saffari 1951 na B. Mapalala1957, E. Mbogo 1947, W. Mkufya.1953, W. K. Wamitila. 1965 N.K. Pili, ni kuongezeka kwa riwaya za kuburudisha na kusisimua, ambako kuliambatana na kuibuka kwa wachapishaji- waandishi kama E. Musiba, B. Mtobwa na E, Shigongo ambao waliandika na kuchapisha riwaya zao wenyewe. Tatu, kujitokeza kwa riwaya iliyohakiki jamii kwa undani. Baadhi ya watunzi mashuhuri wa riwaya hiyo ni: Shafi. A. Shafi Kasiri ya Mwinyi Fuad TPH 1978 na Kuli TPH 1979; S.A. Mohamed Tata za Asumin Longman 1990; E. Kezi lahabi Dunia Uwanja wa Fujo EALB 1975, Gamba la Nyoka EAPL, 1979; C. Mung’ong’o Njozi Iliyopotea TPH 1980; H. Mwakiembe Pepo ya Mabwege Longman Tz 1980, C. S. Chachage Sudi ya Yohana, DUP 1981 na Kivuli DUP 1981; N. Tengambwage Duka la Kaya, Tausi Publishers 1985; Z. Burhani  Mwisho wa Kosa Longman 1987 na G. Ruhumbika Miradi Bubu ya Wazalendo  TPH 1992 . Shafi Vuta N’Kuvute 1998 na Haini 2003, C.S. Chachage Makuad wa Soko Huria 2002.  Nchini Tanzania wakati riwaya hakiki nyingi za kabla ya 1990 zilihakiki mapinduzi ya Zanzibar na matokeo yake Shafi, Said na Ahmed, na pia sera ya ujamaa na utekelezaji wake Kezilahabi, Ruhumbika na Mwakyembe, riwaya za baada ya mwaka 1990 zilitoka nje ya ujamaa na kuangalia ubepari kwa jicho la uchokonozi Ruhumbika na E.Mbogo, na  kusaili utawala wa kidhalimu ( Shafi). Kuzuka kwa utandawazi wa kitamaduni na kiuchumi kuliibua riwaya zilizouchambua mwenendo wa utandawazi na athari zake (Mkufya, Chachage). 
Jambo la nne, ni kuzuka kwa riwaya ya historia. Watunzi mahiri wa riwaya hizo ni B. Mapalala Kwa Heri iselamagazi TPH 1992, G. Ruhumbika Miradi Bubu ya Wazalendo, na Shafi Kuli. Tano, ni kuongezeka kwa riwaya za vijana na watoto. Mfano P. Shija Mashujaa wa Kazakamba na Vijana jasiri, wimbo wa sokomoko, n.k. Sita ni kuzuka kwa riwaya ya wanakisomo: mfano Shaaban. Msuya. Mazungumzo ya Mchana, Mazungumzo ya Usiku, Mazungumzo ya Jioni na Tuzungumze Yajayo na Siri ya Bahati. Saba, ni kuibuka na kuchanua kwa riwaya za Kenya kama tawi maalum linalokua haraka la bunilizi za Kiswahili. Mfano Katamba Mkangi   Walenisi 1995, K.W Wamitila Nguvu ya Sala 1999, Bin –Adam 2002, Msimu wa vipepeo 2007, Tikiti Maji 2013. K. Walibora Siku Njema 1996, Ndoto ya Almasi 2006, Kidagaa Kimemuozea 2012, n.k.


UCHAMBUZI NA UCHANGANUZI WA KAZI YA FASIHI
Uchambuzi na uchanganuzi wa kazi ya fasihi ni ile hali ya kuangalia, kubaini na kutenganisha kazi ya fasihi na kazi isiyo ya kifasihi. Kazi ya fasihi inapoandaliwa huunganishwa na kazi isiyo ya kifasihi ili kumtaka mwanafasihi kuchambua kazi ya kifasihi anayoiona ka kuacha kazi isiyo ya kifasihi katika kazi nzima. Kitendo cha kufanya kazi hiyo ndicho kinaitwa uchambuzi na uchanganuzi wa kazi ya fasihi. Kwa kawaida fasihi imeundwa na vipengele vikuu viwili ambavyo ni fani na maudhui. Vipengele hivi ndiyo vinavyotakiwa kuchambuliwa na mwanafasihi. Vipengele hivi vya fani na maudhui navyo kila kimoja kina vipengele vidogo vidogo ndani yake.  Kabla ya kuona kuwa fani na maudhui vimeundwa na vitu gani hebu kwanza tuone dhana ya fani na maudhui. 

FANI
Neno fani lina tafsiri nyingi zenye kuwakilisha maana ile ile. Wapo wanaosema kuwa ni ufuni wa kisanaa anaotumia msanii katika kufikisha ujumbe wake kwa jamii inayohusika. Wengine wanasema ni umbo lililosarifiwa ili kuelezea hisia za fanani yaani ni ule uzuri, ustadi au ufundi wenye kuleta mvuto maalumu kwa hadhira. Pia wapo wanaosema kuwa ni umbo la nje la kazi ya fasihi inayoelezea maudhui. Kutokana na fafsiri hizi tunaweza kusema kuwa fani ni chombo cha kubebea maudhui kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa hadhira.
Vipengele vya fani
Ndani ya fani kuna muundo, mtindo, wahusika, mandhari, matumizi lugha, jina la kitabu, picha na taswira na ucheshi.

Muundo: Ni namna kazi ya fasihi ilivyosukwa yaani ilivyogawanywa, mririko na mpangilio wa kazi hiyo kwa upande wa visa na matukio kama ni hadithi au tamthilia, na mpangilio wa beti, vina na mizani iwapo ni ushairi. Muundo ndicho kipengele kinachotofautisha utanzu mmoja wa fasihi na mwingine. Mfano muundo wa hadithi katika fasihi simulizi ni wa moja kwa moja wakati muundo wa hadithi katika fasihi andishi unaweza kuwa wa moja kwa moja, rukia au kioo.
Katika fasihi andishi muundo huonesha jinsi mwandishi wa kazi ya fasihi anavyofuma, anavyounda na anavyounganisha tukio moja na jingine, kitendo kimoja na kingine, wazo na wazo sura moja na nyingine, ubeti na ubeti. Katika utanzu wa riwaya na tamthilia ipo miundo ya aina tatu ambayo ni muundo wa msago, kioo na rukia.
Muundo wa msago ni muundo wa moja kwa moja ambao unafuatilia matukio tangu mwanzo hadi mwisho. Mfano mhusika huzaliwa, hukua, huoa/kuolewa, kuzeeka na kufa. 
Muundo wa kioo ni muundo wa kiuchangamano utumiao mbinu rejeshi ambao huweza kumrudisha nyuma msomaji katika mpangilio wa matukio na kuipeleka mbele hadhira yake mfano mzuri ni Zaka la Damu.
Muundo wa rukia ni muundo ambao visa hurukiana. Katika muundo huu kunakuwa na visa viwili au zaidi ambavyo hurukiana katika kusimuliwa kwake na mwisho wa visa hivi huungana na kujenga kisa kimoja. Mfano mzuri ni Njama.

Mtindo: Ni namna fanani anavyounda kazi yake yaani ni mazoea ya msanii yanayojionesha katika fani ya kazi yake. Mazoea hayo yanaweza kuwa ya kuzungumza au kuandika. Katika fasihi andishi mtindo ni upangaji wa fani na maudhui. Katika fasihi andishi mtindo hujidhihirisha katika matumizi ya lugha, nafsi zilizotumiwa na mtunzi, matumizi ya tanzu zingine za fasihi kama nahau, methali, misemo na ucheshi.
Wahusika: 






DHANA YA UHAKIKI 
Uhakiki ni sayansi maalum ya kuchambua na kuona ubora wa kazi ya fasihi kwa kutumia vipengele vya fani na maudhui. Ni elimu na ujuzi ya kuipembua kazi ya sanaa kwa undani na kuyaweka wazi masuala ya msingi yanayoyojitokeza katika kazi ya sanaa kuhusu fani na maudhui. Mchambuzi wa kazi ya fasihi huchambua vipengele viwili yaani fani na maudhui. Uhakiki huwalenga watu wa aina tatu yaani wasomaji wa kawaida walioko shuleni na nyumbani, watunzi asilia wa kazi ya fasihi na wahakiki. Mtunzi hupata faraja na hamasa kutokana na uhakiki wa kazi zake, hukua na kukomaa.
DHANA YA MHAKIKI
Mhakiki ni mchambuzi na mfafanuzi wa kazi ya fasihi. Ni jicho la jamii kwa vile anagundua mazuri na mabaya yaliyomo katika kazi ya fasihi pia ndiye anayeona hatari ya kazi ya fasihi kwa jamii. Mhakiki ni bingwa wa kusikiliza au kusoma na kuchambua maudhui, maadili na ujumbe uliomo katika kazi ya fasihi.
Sifa za mhakiki
Mhakiki anatakiwa ajue historian ya mazingira yaliyomkuza fanani
Mhakiki anatakiwa kujua historia na siasa ya jamii inayohusika. Hii itamwezesha kuyaelewa matatizo ya jamii hiyo
Mhakiki ni muhimu awe amesikiliza au amesoma kazi mbalimbali za fasihi na sio ile tu anayoifanyia kazi. Hii itamsaidia kuwa na ujuzi zaidi katika uwanja wa uhakiki.
Mhakiki anatakiwa tahakiki za wahakiki wengine, katika uwanja wa fasihi na hata nje ya jamii yake ili kupata upanuzi zaidi katika uwanja wa uhakiki
Mhakiki anatakiwa asiwe mpondaji wa kazi za wengine, asichukie au kusifia tu kazi za waandishi kwa sababu zake binafsi bila kueleza ukweli wa kazi hiyo.


DHANA YA TAHAKIKI
Tahakiki ni kitabu kinachotolewa na mhakiki ambacho kinachambua vitabu mbalimbali vya mwaandishi asilia. Tahakiki hutoa uchambuzi na uhakiki wa vitabu vya hadithi, uhairi na drama. Kwa kuzingatia vipengele vya fani na maudhui.
Dhima za mhakiki
Kuchambua na kuweka wazi funzo ambalo linatolewa na kazi ya fasihi
Kuchambua na kufafanua picha za kisanii zilizotumika katika kazi za fasihi
Kumshauri mwandishi ili afanye bora zaidi
Kumwelekeza msomaji ili apate faida zaidi kuliko yale ambayo angeweza kuyapata bila dira ya mhakiki
Kuhimiza na kushirikisha fikra za kihakiki katika kazi ya kifasihi
Kuonyesha kuwa kwa kila kizuri kuna kizuri zaidi na hapana kizuri kisicho dosari
Kutafuta na kuweka sawa nadharia za fasihi teule
Kusema kweli ipasavyo kuhusu tamaduni na falsafa zinazotawala fasihi
Kuheshimu na kuthamini kazi za waandishi za kuzifanyia haki

DHANA YA UDHAMINI KATIKA KAZI YA FASIHI
Udhamini ni hali ya mtu au nchi au shirika fulani kutoa fedha kwa ajili kugharimia kitu fulani. Ni kundi la watu wenye shabaha zinazofanana, wenye kusimama kama wafadhili wa mradi fulani. Katika kazi ya fasihi mdhamini ni mtu au kundi la watu wenye shabaha zinazofanana wenye kusimamia mradi fulani wa kazi ya fasihi kama wafadhili wakiwa na mtazamo wa kipropaganda au kiitikadi.

Aina za udhamini
Kuna aina kuu mbili za udhamini ambazo ni
Udhamini wa ushawishi
Udhamini wa nguvu
Udhamini wa ushawishi
Udhamini wa ushawishi ni udhamini ambao mdhamini anatoa fedha kuwavuta na kuwanunua watunzi wa kazi za fasihi. Matokeo yake ni kwamba mtunzi anafungwa na matakwa ya mdhamini wake.
Udhamini wa nguvu
Udhamini wa nguvu ni udhamini ambao mdhamini anamtaka mtunzi afuate matakwa yake na sio matakwa ya jamii nzima. Mdhamini anaweza akawa mtu binafsi mwenye pesa, shirika, chombo cha serikari, chama fulani au kundi la mataifa kwa ushirikiano. Mdhamini wa namna hii ni mwakilishi wa wenye mamlaka juu yake. Kwa mfano katika Tanzania chuo kikuu ni mwakilishi wa serikali na serikali ni mwakilishi wa tabaka tawala. Hivyo mtunzi anayemilikiwa na udhamini wa aina hii anajikuta anafanya kazi ili kuendeleza maslahi ya tabaka tawala. Kwa kawaida mwandishi akidhaminiwa kwa nguvu huwa kama kasuku aimbaye na kuutukuza mfumo wa maisha uliopo katika jamii hata kama roho na moyo wake viko mbali sana na mfumo huo. 
Kwa nini watunzi wadhaminiwe?
Zipo sababu nyingi sana za kuwafanya watunzi wa kazi ya fasihi wadhaminiwe. Baadhi ya sababu hizi ni pamoja na:
Uhaba wa fedha kwa watunzi za kuendesha shughuli za uandishi. Katika shughuli za uandishi zinahitaji pesa kwa shughuli mbalimbali kama kununua karatasi n.k
Kwa ajili ya kulinda na kutetea maslahi ya wadhamini wao. Hii inatokea sana kama udhamini ni wa tabaka tawala. Kama tabaka linalotawala ni la wafanyakazi, basi shughuli za uandishi zitaongozwa na maslahi na mahitaji ya ya tabaka hilo. Kama tabaka linalotawala ni la kibepari, basi kazi za fasihi zitatetea tabaka hilo.
Kujulikana/ kujipendekeza. Baadhi ya waandishi hudhaminiwa na kwa sababu ya kutaka kujulikana na kwa upande mwingine mdhamini anawadhamini kwa lengo hilohilo.
Baadhi ya waandishi hudhaminiwa kwa lengo la kupata fedha haraka haraka. Hawa huandika kazi ambazo zitaleta pesa ya haraka, mfano riwaya pendwa.
Baadhi ya waandishi hudhaminiwa kwa kulazimishwa na tabaka tawala. Waandishi hawa wanaukubali udhamini huo kwa kuogopa udhibiti wa kazi zao na tabaka tawala. Wandishi hawa wakikataa udhamini huo, kazi zao zitadhibitiwa na kupigwa marufuku zisisomwe au kuchapishwa. 
Pia ifahamike kuwa mdhaminiwa ni mwakilishi wa wenye mamlaka juu yake Mfano katika nchi ya Tanzania baadhi ya Vyuo Vikuu ni mwakilishi wa serikali na serikali ni mwakilishi wa tabaka tawala. Hivyo endapo msanii atadhaminiwa na baadhi ya vyuo hivyo hawezi kuyasema yanayokera katika vyuo hivyo.


UHUSIANO WA MNDAHIMINI NA MTUNZI WA KAZI YA FASIHI
Mdhamini huendeleza watunzi wachanga katika kuchapisha kazi zao na jamii kuweza kuzipata: ili kazi ya mwandishi iweze kufikia lengo lake ni lazima mdhamini aweze kuwadhamini watunzi ili iweze kufikia hadhira iliyokusudiwa.
Mdhamini huweza kumsaidia mtunzi kufanya kazi bora zaidi: kutokana na fedha na vifaa ambavyo mdhamini humsaidia mtunzi wa kazi ya fasihii kufanya kazi bora zaidi na kufanya ifikie jamii husika na kuendeleza ujenzi wa jamii mpya.


UHUSIANO KATI YA MHAKIKI NA MTUNZI WA KAZI YA FASIHI
Wote wanajikita katika kukuza na kuendeleza lugha; mwandishi anapo andika kazi yake hupeleka kwa mhakiki ili ifanyiwe marekebisho hasa katika matumizi ya lugha sanifu, hivyo huibua makosa mbalimbali hivyo kumfanya mtunzi awe imara na kuboreshaa kazi zake zingine, hivyo kuifanya lugha kukua na kuendeleza lugha.
Mhakiki hueleza ubora na udhaifu wa kazi ya mtunzi; hivyo kuweza kuendeleza kazi ya mtunzi iwe bora zaidi kwa jamii aliyokusudia kuiandikia, hivyo mhakiki anakuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza lugha, mhakiki ni mhimu sana katika kazi ya fasihi.
Mhakiki humshauri na kumtia moyo mtunzi wa kazi ya fasihi; hivyo kuongeza hamasa kwa mtunzi wa kazi ya fasihi kuweza kutunga kazi bora zaidi ya ile ya mwanzo.
Mhakiki na mtunzi husaidia kukuza kiwango cha kazi ya fasihi: mhakiki anapo hakiki kazi ya fasihi huweza kuibua makosa na udhaifu wa kazi ya mtunzi, hivyo mtunzi hurekebisha makosa yaliyoibuliwa na mhakiki hii humsaidia mtunzi kuweza kutunga kazi zenye kiwango cha hali ya juu kuliko zile za mwanzo, hivyo huonekana uhusiano mkubwa wa mhakiki na mtuzi wa kazi ya fasihi.

MTUNZI WA KAZI YA FASIHI.
    Ni mtu yoyote anaye jishughulisha na uandishi, utungaji wa kazi ya fasihi yani fasihi andishi na fasihi simulizi ambapo fasihi andishi ni kama vile Ushairi, Tamthiliya na Riwaya. Lengo kubwa la kutunga kazi hizi ni kuelimisha, kuonya, kukemea na kuiadabisha jamii juu ya mambo mbalimbali yanayofanyika katika jamii pia na kutoa masuruhisho mbadal juu ya matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii husika.
MWANDISHI: - Ni mtu yeyote atumiaye muda wake mwingi kuandika na kuzungumza na jamii yake kwa njia ya maandishi.


UHURU WA MTUNZI
     Ni ile hali ya mwandishi wa fasihi kuwa huru na wazi katika kutoa mawazo yake au hisia zake kwa jamii inayohusika bila kupingwa na tabaka lolote katika jamii. Ni uhuru wa kuweza kuandika na kuosoa tabaka lolote katika jamii bila kupata matatizo yeyote.
    Dhana ya uhuru wa mwandishi ni pan asana. Kama uhuru wa mwandishi umo katika utashi. Bila utashi mwandishi atakuwa mwoga na mwepesi wa kukata tama. Atayumbishwa haraka kutoka kwenye msingi wa falsafa yake na imani aliyo nayo juu ya mabadiliko yatokeayo katika jamii. Makambora ya wahakiki na wanasiasa huweza kumyumbisha lakini kwa mwandishi mwenye utashi Makombola hayo humkomaza.

Mfano,
    Wandishi walionyesha utashi wao katika Afrika ni wale Soyinka na Ngungi wa Thiongo. Kwani waandishi hawa wameshambuliwa sana na wahakiki lakini misimamo yao ni ileile kutokana na utashi na falsafa zao.


MAMBO YANAYOFANYA KUWEPO KWA UHURU WA MWANDISHI.
Kwa mujibu wa Kezilahabi Uhuru wa mwandishi unajibainisha katika mambo yafuatayo;

UTASHI
Ni hali ya kuamua, kuazimia au kukusudia jambo bila ya kushurufishwa au kuyumbishwa. Dhima ya mtunzi ni kuamsha jamii iweze kutambua unyonyaji, ukandamizaji na uonevu unaoendelea katikati yake. Ili aweze kuyaeleza haya hutumia utashi wake na kuyaonyesha katika kazi zako kwa wazi au lugha za mficho mfano Ngungi wa Thiongo aliwahi kufungwa na tabaka tawala kutokana na kukosoa uozo wa tabaka hilo.

FALSAFA.
Ni hali ya mtunzi kuwa na msimamo mmoja katika kazi zake. Mfano kama ni uonevu basi kazi zake zitahusu misimamo ya uonevu lakini anapokosa falsafa hujikuta anayumbishwa kutokana na mazingira leo ataandika kuhusu rushwa kesho atazungumzia mapenzi.

SANAA.
Kila utanzu wa fasihi iwe riwaya, ushairi au tamthiliya una mbinu zake. Kwa mfano mwandishi anataka kufikisha ujumbe wake kwa njia ya riwaya ni lazima ajue misingi ya uandishi wa riwaya na ni lazima mwandishi awe mueledi wa misingi ya aina ya sanaa anayotaka kutumia, mwandishi atakuwa na chakusema lakini atashindwa kutokana na weledi mdogo.

LUGHA
Lugha ndiyo malighafi ya kiwanda cha matumizi yake. Mwandishi ambae hana uelewa wa lugha ambayo inazalisha kazi za kifasihi ambayo ni akili yake. Mwandishi atakutana na kizuizi kwa maana kuwa hatakuwa na uhuru wa kusema kile kilicho nafsini mwake kutokana na lugha yake. Mara nyingi mwandishi hutumia lugha za mficho anapokuwa anaeleza mambo yanayoikabili jamii yake ambayo huenda yanasababishwa na serikali ama tabaka tawala lolote ili kuepuka kufungiwa kwa kazi yake.


JE, KUNA UHURU WA MWANDISHI AU MTUNZI WA KAZI YA FASIHI?
        Uhuru wa mwandishi unakuwepo ikiwa hakufaulu kudhuru tabaka tawala. Hii ni kwa sababu suala la uhuru wa mwandishi ni la kitabaka na lilianza pale jamii ilipogawanyika katika matabaka. Kwa maana hii uhuru wa mwandishi unaamuliwa na tabaka tawala.
       Kuanzia enzi za utumwa, maandishi yaliyovumbuliwa yaani fasihi andishi ya mwanzo ilikuwa ya wateule wachache tu na wenye vyeo vyao. Hao mabwana, mamwinyi na mabepari walihakikisha kila mbinu ilitumika ikiwemo ya udhibiti wa mwandishi ili kuendeleza na kulinda utawala wao. Hadi sasa suala hilo lipo kutokana na utawala uliopo.
Kutokana na maelezo hayo inaonyesha kuwa hakuna uhuru wa mwandishi katika jamii ya kitabaka. Hii ni kwa sababu katika jamii hii fasihi ni mali ya tabaka tawala kamwe hakuna fasihi iliyo mali ya jamii nzima.
Fasihi ni mojawapo ya vyombo vya kiitikadi na tabaka tawala daima huhakikisha kuwa chombo hiki hutumiwa kueneza itikadi zake pale fasihi inapojaribu kujitenga au kupinga itikadi za tabaka tawala inakumbana na udhibiti kwa hali hiyo inaonyesha kuwa tabaka tawala ndilo linaloamua juu ya uhuru wa mwandishi na mwandishi akienda kinyume na matakwa ya tabaka tawala lazima atadhibitiwa na tabaka hilo. 
Mfano.
Kuwepo kwa udhibiti katika mfumo wa kibepaari ambapo mshairi maarufu wa Marekani ya kusini, Pablo Neruda ambaye hapo mwanzo aliandika mashairi yanayosifu uzuri wa maua, na machweo ya jua, utume wa nyimbo zitokanazo na mtiririko wa maji maudhui haya yalisifiwa sana na wahakiki wa vyombo vya habari vya kibepari. Lakini baada ya muda Neruda alikubali mwelekeo wake wa maudhui akaanza kuandika utetezi wa mtu mnyonge wa tabaka la chini. Wahakiki waliomsifu mwanzoni sasa walimkashifu na kudai kuwa ushairi wake ulikuwa umepotoka na Neruda alikuwa amechanganya ushairi na siasa jambo ambalo ni mwiko kwa tabaka la kibepari.
Katika Afrika kuna mifano mingi ya udhibiti wa mwandishi mfano mzuri ni kwa mwandishi maarufu wa Kenya Ngungi wa Thiong’o ambaye kazi zake hasa ya Ngaatuka Ndeenda (I will marry when I want – Nitaolewa nikitaka) Iligonganisha vyombo vya dola hadi akawekwa kizuizini kutokana na kufichua siri za mfumo wazi wa kibepari kwa watu wanyonge. Ikaonekana ameudhi tabaka tawala la jamii yake ambalo halikuhusika kutumia udhibiti wa vyombo vyake kwa mabavu.
Kwa upande wa Tanzania udhibiti wa mwandishi ulianza wakati wa ukoloni. Udhibiti huo ulionekana hata katika uteuzi wa vitabu vya kutafsiriwa vilivyoeleza na kutukuza utamaduni wa kwao pamoja na nguvu walizokuwanazo. Vitabu kama vile Vyama shimo ya Mfalme Suileman, Safari za Gullivar na Robinson Kruso viliteuliwa na kutumiwa shuleni kwa malengo maalum. mfano katika robinson kruso mwanafunzi wa kitanganyika alitakiwa akiri nguvu za mzungu mmoja mwenye uwezo wa kutawala kisiwa peke yake  na kuyamudu maisha bila matatizo. haya yote yaliambatanishwa na itikadi na imani za dini ngeni walizowalazimisha watanganyika kuzikubali na kuzitupilia mbali dini na imani zao za jadi. katika kipndi hichoi cha ukoloni, ni dhahiri kwamba udhibiti usingeweza kuyakubali maandishi yanayo pingana na utawala.
        Baada ya uhuru vitabu vingi sana viliandikwa na udhibiti wa maandishi mbalimbali ulijitokeza wazi wazi .mfano E.Kezilahabi aliandika riwya ya Rosa Mistika (1971) kitabu hiki kilipigwa marufuku kisitumiwe shuleni na hata kisiuzwe waziwazi madukani.ilidaiwa kuwa walikipiga marufuku kwa kuwa kilikiuka maadili ya jamii kwa kueleza mambo ya aibu kwa wazi.vile vile hadi sasa udhibiti wa waandishi na watunzi wa kazi ya fasihi umekua mkubwa mno kutokana na kazi zao zinaonekana kukiuka matakwa ya utawala.


DHIMA YA UHURU WA MWANDISHI
Mwandishi ana dhima ya kukosoa jamii au tabaka lolote linaloenda kinyume na utaratibu      wa jamii yake bila matatizo mwandishi atakuwa huru kuonyesha dhuluma, ukatili na ujahili unaofanywa katika jamii na tabaka lolote bila matatizo yoyote. 
Mwandishi hutoa muongozo katika jamii kwa kukomboa jamii kutoka katika fikra mbovu, kugandamizwa, kunyanyaswa na kuonewa na tabaka tawala ili jamii ipate haki na heshima bila woga wa kuliogopa tabaka tawala ambalo ndilo lenye mamlaka yote katika jamii.

Kuwepo kwa uhuru wa mwandishi kunamsaidia msanii kuwa na falsafa inayoeleweka pamoja na utashi wake hii inamfanya mwandishi awe na msimamo unaoeleweka, msimamo wake utamsaidia kuielimisha jamii bila uoga. Ataijulisha jamii hali yake na ataonyesha jamii njia za kufika haja na kutatua matatizo ya jamii bila uoga.
Uhuru wa mwandishi husaidia kupunguza uandishi wa kikasuku. Waandishi au wasanii wanapokuwa huru huacha tabia ya kuwa vipaza sauti vya tabaka Fulani katika jamii wasanii makasuku huandika mambo bila kufikiri na kurudia mawazo yaliyokwisha semwa na wanasiasa majukwaani bila frikra mpya kwa hali hii hupelekea kuipotosha jamii. Hivyo anapokuwa na uhuru, mwandishi unamsaidia kuandika mambo mbalimbali yanayojitokeza katika jamii na kutoweza kujikomba au kujipendekeza kwa tabaka tawala lenye mamlaka yote katika jamii.
Mwandishi atakuwa huru kuelimisha na kuishauli jamii katika mambo muhimu yanayo jitokeza katika jamii bila woga. Mwandishi ataishauri jamii kuhusiana na mambo kama vile afya, elimu na aichunguze ni mambo gani yanafaa kuhifadhiwa. Vile vile msanii anakuwa huru kuilekebisha jamii bila woga kwa kuangalia yapi ni mazuri na yapi ni maovu yanayotendeka katika jamii.


VIKWAZO VYA UHURU WA MWANDISHI 
Udhibiti; Ni mojawapo ya matatizo makubwa ambayo yamekuwa yakiwakumba waandishi wengi ulimwenguni sera ya udhibiti imewahi kuwaathiri waandishi kama vile Sulma Rashid, Wole Soyinka, Euphrase Kezilahabi na hata Ngungi Wa Thiong’o hii hutokea pale ambapo vyombo vya dola hupiga marufuku kazi zao za waandishi kwa kisingizio kwamba hazifai kusomwa na hadhira kwa kisingizio kwamba zinauchafu au zinauchochezi wa aina Fulani unaoweza kuzua zogo na migogogro katika jamii mfano. Riwaya ya Kezilahabi, na Rosa Mistika zilipigwa marufuku kuwa maandiko yao yasisomwe katika kazi mbalimbali za kielimu nchini Tanzania kwa kisingizio kwamba zilikuwa ni chafu.
Tatizo la pili huanzia kwa wachapaji; kama hujulikani kwenye uwanja wa uandishi kazi yako haiangaliwi kwa undani sana na mhariri katika shirika la uchapishaji mswaada huchukua muda mwingi kutathmini (mahojiano kwa njia ya barua pepe)
Ukosefu wa soko; ni tatizo lingine linalowakabili waandishi wa vitabu vya Kiswahili iwapo mwandishi atachapisha kazi yake na kazi hiyo haina nafasi katika mfumo wa elimu hasa shule za msingi na pili huenda asipate mauzo mengi hili ni kwa sababu ya mfumo wa elimu nchini Tanzania.
Uandishi ni taaluma inayohitaji muda mwingi: waandishi wa kazi ya fasihi ni waalimu wanaofundisha katika ngazi mbalimbali katika mfumo wa elimu, mara nyingi waalimu huwa na kazi nyingi kama vile kufundisha, kusahihisha na kusimamia kazi za wanafunzi miongoni mwa nyingine. Muda kwao huwa haba na kushindwa kufikia malengo yao ya taaluma hii, kwa sababu taaluma ya uandishi huhitaji muda mwingi sana.
Katika uandishi wa vitabu suala la utafiti ni muhimu na lazima: Baadhi ya waandishi au watunzi wa kazi za fasihi hawajaaminika katika mbinu za utafiti isitoshe marejeo muhimu ni tatizo kubwa kwa waandishi wa Kiswahili hivyo kazi hushindwa kuendelea.
Kutopata ushauri ufaao kuhusu taaluma ya uandishi na masuala yanayohusu uchapishaji; (Mung’ong’o 1993) Akitoa mfano jinsi kazi yake ilivyokawia kuchapishwa kwa sababu ya kukosa ushauri kazi yangu ya awali kabisa ilikuwa mirathi ya hatari “kazi hii ilianza kuandikwa mapema mwaka wa 1966 nilipokuwa kidato cha pili katka shule ya sekondari kibana lakini kwa sababu ya mzigo wa masomo na kwamba wakati ule sikuwa na mtu wa kunishauri hivyo kazi iliyochukua mda mrefu hadi mwaka 1979.”
Ukosefu wa vifaa vya kisasa vya uandishi: kama vile kompyuta vifaa hivi vya tarakilishi ni ghali mno ingawa ni muhimu sana katika taaluma ya uandishi. Hivyo waandishi wengi hushindwa kuvipata vifaa hivyo na kushindwa kuendelea kwa kazi ya uandishi.





MAREJEO
Madumulla, J.S. (2009), Riwaya ya Kiswahili, Historia na Misingi ya Uchambuzi. Nairobi: Sitima Printer and stations L.td.

Mulokozi, M.M. (2017), Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili.Dar es Salaam.TUKI.
Mhando, P. na Balisidya, (1976), Fasihi na Sanaa za Maonyesho. Dar es Salaam: Tanzania Publishing House. 

Nkwera, F.V. (1978), Sarufi na Fasihi Sekondari na Vyuo.Dar es Salaam: Tanzani Publishing House.






 




 
















 



Comments

Popular posts from this blog

Uchambuzi wa riwaya ya Barua Ndefu Kama Hii